Katika Picha ni Mbunge wa viti maalumu Mkoa wa Njombe Dk Pindi Chana, mgeni Rasmi katika mahafali ya arobaini na sita(46) shule ya msingi Manga Halmashauri ya Mji Makambako,Hafla ambayo imehudhuriwa na Diwani kata ya Mahongole Ndg Mario Kihombo,Diwani viti maalum na mlezi wa kata ya Mahongole Angelina Kimbawala,Mwakilishi kutoka ofisi ya Mkurugenzi Halmshauri ya Mji Makambako Yusto Nyamle,Walimu,Wazazi,walezi na wahitimu wa shule hiyo.
Akizungumza katika hafla hiyo Dk Pindi Chana amewashukuru walimu na wazazi kwa ushirikano wao kwa kufanikisha wanafunzi hao kuhitimu miaka saba(7) ya elimu ya msingi kwa ushirikiano mkubwa ,mshikimano upendo na mwamko wa kusukuma gurudumu la elimu hapa nchini kwa ngazi ya Halmashauri ,Mkoa mpaka Taifa.
"Niwaombe wazazi na walezi tushirikiane kuwalea watoto wetu hawa na kuwatunza kwa ukaribu mkubwa hasa kipindi hiki wanaposubiri matokeo yao ya kujiunga na elimu ya sekondari ,kwani huko mtaani watoto hawa wanasubiliwa kama simba aliye na njaa kali mawindoni hivyo basi tuache mipango ya kuwasafirisha wanafunzi hawa kwenda mijini kufanya kazi za ndani kwani bado wadogo sana kikubwa wazazi jiandaeni kuwapeleka watoto elimu ya sekondari ,amesema Dk Pindi.
Ameongeza pia elimu ndio kila kitu na ni urithi wa pekee kwa mtoto elimu ya darasa la saba ni sawa na mbegu ya mche inayoaanza kumea safari ya elimu bado ni ndefu kwao hivyo serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ipo pamoja na walimu ,wazazi na walezi pia hususani katika kuendelea kutatua changamoto zinazoikumba sekta ya elimu nchini ndio maana kwa mwaka wa fedha 2021-2022 serikali ya Mama Samia Suluhu Hasan imeshatoa fedha kwaajili ya kutatua changomoto kwa shule mbalimbali za msingi nchini hasa vyumba vya madarasa na shule ya Msingi Manga ni moja wapo.
Akitoa salamu za Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Makambako Mwakilishi wa Mkurugenzi,Yusto Nyamle amesema katika suala la elimu kwa Halmashauri ya Mji wa Makambako kimkoa si haba kwani tangu Mkoa wa Njombe kuanzishwa Halmashauri ya Mji Makambako imekua ikifanya vizuri kielimu na michezo pia.
Katika suala zima la changamoto katika shule za msingi Halmashauri ya Mji Makambako amesema kwa kila shule tayari ofisi ya Mkurugenzi inaendelea kufanyia kazi changamoto mbalimbali hususani vyumba vya madarasa hivyo ushirikiano mkubwa unahitajika kwakuwa umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu hasa katika kusukuma gurudumu la elimu kwa ngazi ya Halmashauri, Mkoa na taifa.
Mwisho Mbunge viti maalumu Dk pindi Chana amesema kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Njombe anaishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwasaidia wakulima katika soko la Mahindi kwani wakulima wengi wa zao hilo walikuwa wamekata tamaa sana hususani katika Mikoa inayozalisha mahindi kwa wingi ikiwemo Mkoa wa Njombe.
Serikali yetu ni sikivu sana wakulima sasa mahindi yao yatauzwa kwa bei nzuri ,niwaombe wana Njombe tushirikiane tudumishe amani upendo kwani amani tuliyo nayo yapo mataifa yanaitamani ,wapo watu hawana muda hata wa kukaa pamoja na kuzungumza masuala ya maendeleo kwahiyo tuitunze Lulu hii,na Katika changamoto ambayo imesomwa katika risala ya shule hiyo hususani ukosefu wa vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) amesema ameipokea changamoto hiyo na ataifanyia kazi kwani kwa ulimwengu wa sasa TEHAMA ndio Msingi wa Taifa lolote endelevu.
kazi iendelee.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa