Na. Lina Sanga
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Mji Makambako leo,limepitisha Rasimu ya Mpango na Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2022/2023 yenye Jumla ya Shilingi bil. 25.9, ili kuiwezesha Halmashauri ya Mji Makambako kutekeleza shughuli mbalimbali za kiutalawa na kiutendaji pamoja na utekelezaji wa miradi ya maendeleo na Jumla ya shilingi Mil. 700 ikiwa ni uchangiaji wa nguvu za Wananchi kwenye Miradi ya Maendeleo.
Akiwasilisha Rasimu hiyo Afisa Mipango wa Halmashauri ya Mji Makambako, Bw. Eliud Mwakibombaki amesema kuwa Halmashauri imeomba kuidhinishiwa kiasi hicho cha fedha,ikiwa shilingi Bil. 15.1 ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi, shilingi Bil. 2.6 Kwa ajili ya matumizi mengine na shilingi Bil. 8.2 kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Makambako,Bw. Kenneth Haule amesema kuwa Halmashauri kwa sasa inatarajia kuanzisha miradi mbalimbali ili kuongeza makusanyo ya mapato ya halmashauri ikiwa ni pamoja na kuanzisha maegesho ya malori katika Kata ya Majengo na Mradi wa kufyatua tofali.
Haule amesema kuwa halmashauri inatakiwa kukusanya jumla ya shilingi bil. 2.7 ikiwa ni mapato ya ndani,na mapato hayo yanakusanywa ngazi ya Kata na ngazi ya Halmashauri katika vyanzo vya mapato vinavyotambulika kisheria na sio idadi ya watu waliopo kwenye Kata husika.
“Ukusanyaji wa mapato hauzingatii idadi ya watu bali vyanzo vinavyotambuliwa kisheria,lakini mgao wa mapato unafanyika kwa kuzingatia idadi ya watu ,hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kulipa kodi na ushuru wa mapato wa Halmashauri kama sheria inavyotaka na watendaji wa Kata,Mitaa na Vijiji wanawajibu wa kukusanya mapato ili Bajeti ya Halmashauri iongezeke”,alisema Haule.
Aidha, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Makambako, Bw. Hanana Mfikwa ametoa wito kwa Halmashauri kuendelea kutafuta vyanzo vya mapato,ili kuongeza makusanyo ya mapato ambayo yatasaidia kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa shule na huduma mbalimbali za kijamii.
Wakati huo huo, Katibu Tawala Wilaya ya Njombe, Bw. George Emmanuel amepongeza Baraza la Madiwani kwa kupitisha Rasimu ya Mpango na Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2022/2023,lakini pia amewataka wananchi wote wa Halmashauri ya Mji Makambako kujitokeza kushiriki Zoezi la Uwekaji wa Anwani za Makazi,Uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru ambapo kwa mwaka huu utafanyika Mkoa wa Njombe sambamba na zoezi la Sensa za Watu na Makazi linalotarajiwa kufanyika Mwezi Agosti Mwaka huu Nchi nzima.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa