Jumla ya bil.429.1 zimetolewa na Serikali kwa ajili ya kufanya maboresho ya bandari ya Tanga,ili kupunguza gharama za kushusha mizigo baharini na uendeshaji wa operesheni,ambapo jumla ya bil.256.8 zimetolewa na serikali awamu ya pili ili kufanya upanuzi wa bandari kwa kujenga gati mbili zenye upana wa mita 150 na urefu wa mita 450 ,na bil.172.3 zilitolewa awamu ya kwanza kwa ajili ya kuongeza kina cha bahari na lango la kuingilia bahari.
Taarifa hiyo imetolewa na Mhandisi wa bandari ya Tanga,Mhandisi Khamis Omary Kipalo wakati akizungumza na Mkurugenzi wa Idara ya habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa katika ziara ya Maafisa habari,Mawasiliano na Uhusiano wa Serikali iliyofanyika leo katika bandari hiyo ili kutembelea mradi wa ujenzi wa gati za kushushia mizigo zinajengwa na kampuni ya China Urban Co.Ltd.
Mhandisi Kipalo amesema kuwa maboresho ya bandari ya Tanga yamefanyika kwa awamu mbili ambapo katika awamu ya kwanza kazi zilizofanyika ni kuongeza kina kwenye lango la bahari na kuchimba eneo la kuingilia bahari na kugharimu jumla ya shilingi Mil. 172.8 na mradi umekamilika kwa asilimia 98.
"Serikali imeamua kutoa fedha hizo ili kupunguza umbali wa kufuata mizigo baharini kutokana na kukosekana kwa gati za kushushia mizigo katika bandari hii,na gharama za utekelezaji wa operesheni zilikua kubwa sana tofauti na sasa baada ya umbali wa kushusha mizigo kupungua",alisema Kipalo
Amesema kuwa zamani meli ilipowasili mzigo ulifuatwa kwa umbali wa kilomita 1.7 kutoka bandarini,lakini baada ya Serikali kuamua kuongeza kina cha kuingia kwenye lango la bahari umbali kufuata mizigo umepungua na kufika mita 200 kutoka bandarini na gharama za uendeshaji wa operesheni zimepungua.
Naye Mkurugenzi wa idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu Wa Seriikali, Gerson Msigwa amesema kuwa endapo mradi huo ukikamilika utapunguza gharama za kushusha mizigo na wananchi watanufaika kupitia bandari hiyo na kupunguza msongamano wa mizigo katika bandari ya Dar es salaam kwani nchi jirani kama Rwanda,Burundi,Uganda na Kongo zinaweza kutumia bandari ya Tanga.
Amebainisha kuwa bandari ya Dar es salaam jumla ya trilioni moja inatumika kupanua njia ya kupita meli kubwa,lakini pia bandari mbalimbali ikiwemo bandari ya Kalema imefikia asilimia 90,bandari ya mtwara maboresho yamefanyika na sasa imekamilika na ina uwezo wa kuhudumia tani milioni moja kwa mwaka,na serikali inafanya jitihada ya kuunganisha kutoka Mtwara,Mbamba bay na kuhudumia Nchi ya Malawi.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa