Na. Lina Sanga
Bi. Alatwimika Mlawa,mkazi wa Kitongoji cha Isaula katika Kijiji cha Ibatu,Kata ya Kitandililo ameishukuru Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya jamii –TASAF,kwa kumuwezesha fedha na mradi wa nguruwe ambao sasa unamsaidia kupata matibabu ya moyo.
Bi. Alatwimika,ambaye ni mnufaika wa TASAF tangu mwaka 2015 kwa sasa anasumbuliwa na ugonjwa wa moyo kutanuka uliomuanza mwezi februari mwaka huu, na kumfanya ashindwe kufanya shughuli yoyote ya kumuingizia kipato.
Amesema kuwa, kupitia TASAF alipewa mradi wa ufugaji wa nguruwe uliomuwezesha kupata jumla ya shilingi 500,000 kwa kuuza vitoto vya nguruwe kumi,na kufanikiwa kununua ng’ombe ambaye alimuuza baada ya kuugua ili aweze kupata matibabu.
“Mwaka huu mwezi wa pili nilianza kuumwa ndipo nilipogundulika nina tatizo la moyo kutanuka,ikanibidi niuze ng’ombe niliyemnunua ili niweze kukidhi gharama za matibabu yangu,naishukuru sana Serikali maana bila TASAF ningekuwa nimefariki mwezi wa pili kwa kukosa hela ya kulipia huduma ya matibabu,nipo hai kwa sababu ya TASAF ingawa siwezi tena kufanya kazi nilizokuwa nafanya awali”,alisema Bi. Alatwimika.
Licha ya ugonjwa unaomkabili Bi. Alatwimike hajakata tama ya kuendeleza mradi wa ufugaji wa nguruwe aliopewa na TASAF , kwani hadi hivi sasa ana nguruwe dume mmoja wa mbegu anayemkodisha kwa wengine na kulipwa kitoto cha nguruwe kimoja kila baada ya nguruwe hao kuzaa.
Aidha, kupitia fedha anazopewa na TASAF kila ya miezi mitatu zinamuwezesha kulipa vibarua wanaomfanyia kazi za shamba na matumii ya nyumbani.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa