Na. Lina Sanga
Bodi ya chuo kikuu cha Mwalimu Nyerere leo imetembelea eneo la ujenzi wa chuo hicho katika Halmashauri ya Mji Makambako lenye ukubwa wa ekari 103,huku wananchi wakitakiwa kuchangamkia fursa mbalimbali pindi ujenzi utakapoanza kwa kujenga hosteli kwa ajili ya wanafunzi na miundombinu mingine kwa ubia(PPP).
Makamu Mwenyekiti wa bodi hiyo,Bi. Fatuma Ramadhani amesema kuwa bodi imeridhishwa na eneo hilo na kuahidi kushirikiana na viongozi wa chuo hicho kufikia lengo lililokusudiwa,ili kutoa huduma ya elimu kwa wakazi wa Makambako na maeneo jirani.
Prof. Haruni Mapesa, Mkuu wa chuo hicho ameishukuru Halmashauri kwa kutoa eneo bure na kusema kuwa ndani ya miaka mitatu wataanza programu za kufundisha ,baada ya ujenzi wa miundombinu ya kujifunzia na ofisi za wafanyakazi kukamilika ,majengo mengine yataongezwa kwa awamu baada ya chuo kuanza.
Ametoa wito kwa wananchi wenye uwezo wa kujenga hosteli kujitokeza pindi ujenzi wa chuo hicho utakapoanza pamoja na kushiriki ujenzi wa baadhi ya miundombinu kwa ubia.
Mkuu wa Wilaya Ya Njombe,Mhe. Juma Sweda ameihakikishia bodi hiyo kuwa Makambako ipo tayari kuupokea mradi wa ujenzi wa chuo kikuu cha Mwalimu Nyerere kwani mradi huo utafungua fursa nyingi zenye manufaa kwa wananchi na Makambako kwa ujumla.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa