Na. Lina Sanga
Chama cha Skauti Halmashauri ya Mji Makambako leo,kimeadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa kwa muasisi wa skauti duniani, Baden Powell raia wa Uingereza kwa kupanda miti ya parachichi shule ya Msingi Mwembetogwa, iliyotolewa na Serikali kwa ajili ya kukuza kipato cha shule na lishe kwa wanafunzi.
Akizungumza baada ya kukamilika kwa zoezi la upandaji miti ,Mwl. Diana Nyemele ambaye ni mwanzilish na mlezi wa skauti Wilaya ya Njombe, ameishukuru Serikali kwa kutoa miche ya parachichi mashuleni na kuwataka wanachama wa Skauti kudumisha amani,upendo na uzalendo kwani lengo kuu la kuanzishwa kwa chama cha skauti ni kujenga vijana wenye ukakamavu,mshikamano na uzalendo kwa manufaa ya jamii na nchi kwa ujumla.
Amesema kuwa,chama cha skauti kilianzishwa mnamo mwaka 2004 katika shule ya Msingi Azimio ,Njombe ikiwa Wilaya chini ya Mkoa wa Iringa ,na baadaye ilienea shule mbalimbali na hadi sasa chama hicho kipo imara na kutoa wito kwa wanafunzi kujiunga na chama cha skauti ,ili waweze kujifunza stadi za maisha na masuala mbalimbali ya ulinzi binafsi na taifa kwa ujumla.
Naye Mwl.Emmanuel Lugongo,Kamishina wa skauti Wilaya ya Njombe ametoa wito kwa vijana ambao wamehitimu masomo na hawana ajira, kujiunga na chama cha skauti na kukiendeleza kiwanda cha utengenezaji chaki,kilichoanzishwa na wanachama wa skauti wa Makambako.
Ametoa wito kwa Walimu wakuu na wamiliki wa shule kuunga mkono juhudi za chama cha skauti kwa kununua chaki, zinazotengenezwa katika kiwanda hicho ili vijana wasio na ajira waendelee kujiajiri.
Tusiwene Mahenge,ambaye ni muasisi wa Chama cha Skauti Mkoa wa Iringa 2004 na Mlezi wa skauti Mkoa wa Njombe kwa sasa,ametoa wito kwa wanafunzi wote ambao ni wanachama wa chama cha skauti kuzingatia masomo na kuhakikisha wanafaulu vizuri,ili kukijengea sifa nzuri chama hicho kwani wengi waliopitia mafunzo ya skauti wamefanikiwa kupata ajira katika kada mbalimbali ikiwa ni pamoja na jeshi.
Chama cha Skauti kilianza rasmi Mwaka 1912 Zanzibar na Mwaka 1917 Tanganyika na Mkoani Njombe mwaka 2004 ikiwa ni Wilaya iliyokuwa chini ya Mkoa wa Iringa.
Maadhimisho ya kumbukizi ya kuzaliwa kwa muasisi wa skauti hufanyika februari 22,kila mwaka ambapo kwa mwaka huu kitaifa maadhimisho hayo yanafanyika jijini Tanga.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa