Na. Tanessa Lyimo
Mkuu wa Wilaya ya Njombe,Mhe. Juma Sweda ameutaka uongozi wa Halmashauri ya Mji Makambako kushirikiana na wafanyabiashara wa Soko kuu na Stendi ya zamani, katika harakati za kuwahamishia kwa muda wafanyabiashara hao katika eneo la kuoshea magari mkabala na A one lodge, lililopo katika Mtaa wa Kahawa, Kata ya Kitisi ili kupisha ujenzi wa Soko la kisasa unaotarajiwa kuanza mwaka ujao wa fedha 2025/2026,kupitia mradi wa uboreshaji miji wa TACTIC.
Mhe. Sweda ametoa rai hiyo leo katika Mkutano wa hadhara na wafanyabiashara wa Soko kuu na Stendi ya zamani , na kumuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Makambako, kuzingatia suala la Miundombinu wakati wa ujenzi wa soko hilo hasa miundombinu ya vyoo.
Aidha,ameuagiza uongozi wa Halmashauri kupitia divisheni ya Biashara,Viwanda na Uwekezaji kuendelea kuboresha mazingira ya wafanyabiashara kwa kutekeleza majukumu yao, ili kusaidia kuongeza mapato na kuleta taswira nzuri ya uwekezaji katika Mji wa Makambako.
Wakati huo huo, Mbunge wa jimbo la Makambako, Mhe. Deo Kasenyenda Sanga amemkaribisha Mhe. Sweda katika jimbo la Makambako baada ya kufanyika kwa mabadiliko ya wakuu wa Wilaya na kumshukuru Dkt.Samia Suluhu Hassan ,kwa kutambua umuhimu wa sekta ya Afya kwa kutoa vifaa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na magari mawili ya kubebea wagonjwa aliyokabidhi leo.
Ndg. Kenneth Haule, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Makambako , amewataka wananchi kupuuza taarifa za upotoshaji kuhusu eneo la muda lililotengwa kwa matumizi ya soko wakati wa ujenzi wa soko jipya, na kuwahakikishia kuwa kila mfanyabiashara anayetambulika na uongozi wa soko hilo atapata nafasi ya kufanya biashara bila kubaguliwa wala kusumbuliwa katika eneo hilo.
Naye, Mwenyekiti wa Jumuiya ya wafanyabiashara Mkoa wa Njombe na Nyanda za juu Kusini,Ndg. Sifael Msigala amemshukuru Mkurugenzi kwa ushirikiano baina ya wafanyabiashara na watendaji wa Serikali, katika mchakato mzima wa maandalizi ya awali katika mageuzi ya soko hilo na katika masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo na changamoto zinazowakabili wafanyabiashara.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa