Na.Lina Sanga
Watendaji wa Kata,Mitaa na Vijiji wametakiwa kuendelea kulinda amani na usalama wa wananchi, ikiwa ni pamoja na kulinda haki na usalama wa watoto ili kutokomeza vitendo vya kikatili katika jamii.
Rai hiyo imetolewa leo na Mwl. Samweli Komba,Afisa elimu awali na Msingi katika Halmashauri ya Mji Makambako wakati akiwasilisha maelekezo kwa Watendaji wa Kata waliohudhuria mafunzo ya shule salama moja kati ya afua nane za mradi wa BOOST yaliyofanyika shule ya Msingi Kahawa.
Mwl. Komba amesema kuwa, Watendaji wana jukumu kubwa la kuhakikisha amani na usalama wa raia na mali zao kwenye maeneo yao,pamoja na kushughulikia migogoro mbalimbali katika jamii ili kutokomeza vitendo vya uvunjifu wa amani na ukatili na uvunjaji wa haki za watoto.
Naye, Bw. Masinde Masinde ,Afisa Ustawi wa jamii Halmashauri ya Mji Makambako amewataka Watendaji wa Kata kufanya mikutano kwenye Kata zao na kuwaelimisha wananchi ,juu ya umuhimu wa utoaji wa taarifa za ukatili dhidi ya watoto na kutoa ushahidi Mahakamani juu ya vitendo vya ukatili dhidi ya watoto kwani ni takwa la kisheria na endapo ikibainika mtu yeyote alificha taarifa hizo kwa maslahi binafsi atashtakiwa kwa mujibu wa sheria.
Amesema kuwa kwa mujibu wa sheria ya kumlinda mtoto,Mamlaka ya Serikali za Mitaa katika kifungu cha 94 ina wajibu wa kumlinda mtoto na kila Mwananchi ana wajibu wa kumlinda mtoto na kutoa taarifa sahihi za ukatili anazofanyiwa mtoto katika familia au jamii husika chini ya kifungu namba 95,na adhabu kwa yeyote asiyetoa taarifa za ukatili anaofanyiwa mtoto ni faini isiyopungua mil.5 au kifungo cha miezi sita au vyote kwa pamoja.
Ametoa wito kwa jamii kutambua kuwa ,suaka la kutoa taarifa za vitendo vya ukatili wa mtoto sio hiyari bali ni lazima kwa mujibu wa sheria,hivyo kila mtu ana wajibu wa kuhakikisha katika familia yake na jamii yake hakuna vitendo vya ukatili kwa watoto na endapo vipo taarifa zitolewe kwa watendaji wa Mitaa,Vijiji na Kata ili sheria ichukue mkondo wake.
Mwl. Exaveria Mtega,Afisa elimu Maalum Halmashauri ya Mji Makambako,ametoa rai kwa watendaji kuanzisha utaratibu wa kuhakikisha wazazi wanawatimizia watoto mahitaji muhimu ikiwa ni pamoja na kufanya ukaguzi wa mahali wanapo lala watoto kila nyumba,kama ambavyo miaka ya nyuma maafisa afya walivyokuwa wanafanya ukaguzi kwani nayo ni moja ya haki ya mtoto kulala mahali pazuri na safi.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa