Na. Lina Sanga
Halmashauri ya Mji Makambako katika bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/2023 imepata jumla ya shilingi Bil. 42 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya Maji na mkataba tayari umesainiwa na mkandarasi.
Hayo yameelezwa na Mbunge wa jimbo la Makambako,Mhe. Deo Kasenyenda Sanga katika mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Mawande, Utengule na Ikelu leo,ikiwa ni sehemu ya ziara ya Mbunge ya kutembelea wananchi na kusikiliza kero zao.
Mhe. Sanga amesema kuwa katika awamu zote za Serikali zilizopita halmashauri ya Mji Makambako haijawahi kupata fedha nyingi kama awamu hii ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya miundombinu ya elimu na Maji.
“Juzi tulikuwa ikulu kushuhudia utiaji saini mikataba ya maji ambapo nimeshuhudia Mkandarasi akisaini Mkataba wa mradi wa Maji wa Halmashauri ya Mji Makambako wenye jumla ya Bil. 42,na hiyo ni sababu inayotufanya sisi kumpongeza Mhe. Samia Suluhu Hassan,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutuona Sisi na kutupatia fedha nyingi kwani haijawai kutokea kupata fedha nyingi kiasi hiki”,alisema Mhe. Sanga.
Ameongeza kuwa jumla ya miji 28 pekee Nchini imepata fedha za utekelezaji wa miradi mikubwa ya maji,Halmashauri ya Mji Makambako ikiwa ni miongoni mwa Miji hiyo,hivyo kupitia miradi hiyo vijana wetu watapata ajira ya kuchimba mitaro na kazi mbalimbali wakati wa ujenzi wa miradi ya maji katika Halmashauri.
Amesema kwa upande wa elimu,ametoa fedha zake binafsi kwa ajili ya kujenga madarasa zaidi ya tisa pamoja na ofisi ili kuunga juhudi za Serikali na wananchi katika kujenga na kuboresha miundombinu ya elimu,hivyo kwa kila mwananchi hana budi kuchangia ujenzi wa madarasa kwani hata kijana ambaye ana mtoto mdogo sasa, anatakiwa kuchangia ujenzi wa madarasa na bweni kwani mtoto wake akikua atatumia madarasa hayo na bweni.
Ameongeza kuwa Serikali imekuwa ikileta fedha kwa ajili ya ujenzi wa majengo mbalimbali katika sekta ya afya na elimu,lakini pia wananchi wanatakiwa kuchangia ili kuona thamani ya majengo hayo kupitia michango mbalimbali.
“Serikali imekuwa na taratibu za kuleta fedha mara kwa mara kwa ajili ya miradi ya ujenzi wa vituo vya afya,zahanati na madarasa,lakini ili kuonyesha uhuitaji wa majengo hayo Serikali inamtaka kila mwananchi kuchangia ili kuonyesha thamani ya jengo linalojengwa iwe kwa kubeba mawe,kusafisha eneo na kazi zingine katika eneo la mradi”,alisema Mhe. Sanga.
Katika kijiji cha Mawande Mhe. Sanga ameahidi kuchangia ujenzi wa shule shikizi katika kitongoji cha Mjimwema ili kuwapunguzia umbali wanafunzi wa kutembea,ambapo jumla ya tofali elfu mbili zitatolewa na mifuko 50 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mawili ya kuanzia.
Katika kuunga juhudi za Serikali na wananchi za ujenzi wa madarasa kwa shule mbalimbali zilizopo Halmashauri ya Mji Makmbako,Mhe. Deo Kasenyenda Sanga kwa mwaka huu amejenga jumla ya madarasa tisa na ofisi mbili ambapo shule ya Kitisi Sekondari madarasa mawili,Shule ya Msingi Mwembetogwa madarasa mawili na ofisi moja, Shule ya Msingi uhuru madarasa mawili,shule ya msingi ilangamoto darasa moja,shule ya msingi shikizi kifumbe madarasa mawili na Ofisi moja.
Pia kupitia wadau ambao ni Asas jumla ya madarasa mawili yamejengwa katika shule ya msingi Magegele na madarasa hayo yapo katika hatua za ukamilishaji na darasa moja katika shule ya Msingi Majengo lilijengwa na aliyekuwa Mbunge wa Mbarali kutokana na ushawishi wa Mhe. Sanga.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa