Na. Lina Sanga
Halmashauri ya Mji Makambako imeshika nafasi ya kwanza awamu tatu mfululizo,katika kampeni za utoaji chanjo ya polio kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano katika Mkoa wa Njombe.
Kauli hiyo imetolewa leo na mratibu wa Chanjo katika Halmashauri ya Mji Makambako, Bi. Tindichebwa Mazala katika kikao cha tathimini ya zoezi la kampeni za chanjo ya polio zilizofanyika awamu tatu na utambulisho wa awamu ya nne ya kampeni ya chanjo ya polio itayoanza kutolewa desemba 1 hadi 4,2022 kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
Tindichebwa amesema kuwa matokeo ya kampeni zilizopita yamefikia lengo ambapo awamu ya kwanza watoto waliopata chanjo ni asilimia 144,awamu ya pili ni asilimia 125 na awamu ya tatu ni asilimia 120, na katika awamu ya nne ambayo ndiyo ya mwisho jumla ya watoto 33,496 wanatarajiwa kupata chanjo hiyo ili kukamilisha dozi.
Amesema kuwa,idadi hiyo ya watoto ambao ni walengwa wa kampeni ya chanjo awamu ya nne, inatokana na idadi ya watoto waliopata chanjo awamu ya tatu.
Ametoa wito kwa wazazi na walezi kuhamasika na kuhakikisha kila mtoto mwenye umri chini ya miaka mitano,anapata chanjo ya polio awamu ya nne ili kupata kinga kamili na kuachana na dhana potofu zilizojengeka katika fikra za baadhi ya watu.
Emmanuel George,Katibu Tawala Wilaya ya Njombe ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya afya ya msingi ametoa rai kwa wataalamu wa afya kuzingatia matumizi ya lugha rahisi,ili waweze kueleweka kwa wazazi na walezi wa watoto wanaotakiwa kupata chanjo hiyo kwa kutoa majibu sahihi juu ya utoaji wa chanjo ya polio kwa awamu nne.
Aidha, amewataka wataalamu wote wa afya wataoshiriki katika zoezi la utoaji chanjo nyumba kwa nyumba,kuwa wabunifu na kuzingatia muda na mazingira ambayo wazazi na walezi wanapatikana ili kihakikisha kila mtoto anapata chanjo hiyo ikibidi wafuatwe shuleni na maeneo mengine walipo kutokana na msimu wa kilimo.
Ametoa rai kwa wajumbe wote wa kikao cha kamati ya afya ya msingi kuhamasisha jamii na familia zenye watoto chini ya umri wa miaka mitano,ili watoto hao wapate chanjo ya polio awamu ya nne na kukamilisha dozi.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa