Na. Lina Sanga
Halmashauri ya Mji Makambako imetakiwa kuendelea kuongeza miundombinu ya elimu hususani nyumba za walimu katika shule zilizopo pembezoni mwa Mji,ili kuwavutia walimu kufanya kazi katika shule hizo na kupunguza uhaba wa walimu shuleni.
Rai hiyo leo na Kamati ya Fedha na Uongozi katika ziara ya ukaguzi wa mradi wa nyumba pacha ya watumishi katika shule ya Msingi Mfumbi,iliyopo Kijiji cha Mfumbi,Kata ya Kitandililo.
Mhe. Odilo Fute,diwani wa Kata ya Mlowa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Fedha na Uongozi,amepongeza ujenzi wa nyumba hiyo ya walimu katika shule hiyo na kusema kuwa, ipo haja ya kuendelea kuongeza na kuboresha mazingira kwenye vijiji vilivyopo pembezoni mwa Mji kama kijiji cha Mfumbi na Wangama hususan nyumba za walimu ili walimu wasihame kwa kukosa nyumba za kuishi.
Amesema kuwa,katika vijiji hivyo hakuna hata nyumba za kupanga pamoja wala usafiri wa uhakika, hivyo mazingira yakiwa mazuri walimu watavutiwa kufanya kazi kwenye shule za Vijiji hivyo.
Aidha,ametoa pongezi kwa Mkurugenzi kupitia idara ya elimu ya awali na msingi na idara ya miundombinu kwa kusimamia vizuri mradi huo kwa viwango vyenye ubora.
Naye,Mwenyekiti wa kjjiji cha Mfumbi ,Juhudi Ng'umbi ametoa pongezi kwa Mkurugenzi kwa kuhamasisha ujenzi wa nyumba ya watumishi na kutoa shukurani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na Mbunge wa jimbo la Makambako,Mhe. Deo K. Sanga kwa kusimamia na kufanikisha zoezi la kusogeza huduma ya umeme katika Kijiji cha Mfumbi na sasa transfoma imefika na umeme utaanza kusambazwa hivi karibuni.
Ujenzi wa nyumba pacha ya watumishi katika shule ya msingi Mfumbi,umegharimu jumla ya Mil. 53.8 na mradi upo hatua za ukamilishaji ambapo hadi kukamilika utagharimu jumla ya Mil. 61.8.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa