Na. Lina Sanga
Jukwaa la wadau wa ustawi wa mtoto limezinduliwa rasmi leo katika Halmashauri ya Mji Makambako,ili kuwawezesha wadau mbalimbali kuchangia mahitaji ya watoto wanaoishi kwenye mazingira hatarishi.
Akizungumza na wadau wa ustawi wa mtoto katika Halmashauri ya Mji Makambako leo,Bw. Erick Haule kwa niaba ya Afisa ustawi wa jamii Mkoa wa Njombe, amesema kuwa lengo kuu la jukwaa hilo ni kutekeleza Mpango wa taifa wa kuhudumia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi wa mwaka 2017 , wenye malengo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuongeza na kuimarisha uwezo wa kaya na jamii kuhudumia watoto waliopo katika mazingira yao.
Amesema kuwa,lengo lingine la jukwaa hilo ni kuongeza upatikanaji na matumizi ya huduma zinazozuia na kuitikia masuala yote yanayohusiana na ukatili wa Kijinsia na ukatili dhidi ya watoto,na kuboresha uwezo wa watoto waliopo katika mazingira hatarishi kuweza kutumia na kupata huduma za elimu,Afya na maendeleo na makuzi yao.
Ametoa rai kwa wadau wa ustawi wa mtoto kuratibu huduma wanazotoa kwa watoto ,ili kujua huduma zinazotolewa kwa watoto hao na kuhakikisha huduma hizo zinawafikia watoto wote wenye uhitaji, na kutambua mazingira wanayoishi watoto kwani ni chanzo kikubwa cha kuongezeka kwa watoto wanaoishi mazingira hatarishi kutokana na kaya zao kukithiri vitendo vya ukatili.
Pia ametoa wito kwa wadau wenye nia ya kutoa huduma kwa watoto kutoa huduma zinazoendana na umri wao,kama viatu,mavazi na kutowapa vyakula vilivyoharibika na visivyofaa kwa matumizi ya binadamu kwa kigezo cha kutoa msaada.
Bi. Appia Mayemba,Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Makambako ametoa wito kwa wadau mbalimbali wa ustawi wa mtoto, katika Halmashauri ya Mji Makambako kujitoa katika kuchangia mahitaji ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi,ili kuwawezesha watoto hao kufikia malengo yao na kuweza kujitegemea.
Jukwaa la wadau la ustawi wa mtoto Mkoa wa Njombe,lilizinduliwa rasmi septemba 29,2023 na Mhe. Anthony Mtaka,Mkuu wa Mkoa wa Njombe kwa kukutanisha wadau mbalimbali ndani ya Mkoa wa Njombe ili kutoa fursa ya uchangiaji na uwezeshaji wa watoto wenye mahitaji mbalimbali.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa