Na. Lina Sanga
Jumla ya lita mil 4.9 za maji zinahitajika katika Halmashauri ya Mji Makambako ili tatizo la uhaba wa maji litoweke na wananchi wote kunufaika na huduma ya maji.
Taarifa hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mjini Makambako (MAKUWASA),Mhandisi Oscar Lufyagile katika Mkutano wa Mbunge wa Jimbo la Makambako,Mhe. Deo Kasenyenda Sanga uliofanyika leo katika Mitaa mitatu na kuzungumza na wananchi wa mitaa saba ya Kata ya Lyamkena,ikiwa ni ziara ya Mbunge kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo na kuzungumza wananchi pamoja na kutoa jumbe mbalimbali za Serikali kama bajeti ya mwaka 2022/2023,Sensa ya watu na Makazi,Mbolea ya ruzuku na chanjo ya Uviko 19.
Mhandisi Lufyagile amesema kuwa,katika Halmashauri ya Mji Makambako jumla ya lita Mil 9.6 za maji zinahitajika,lita za maji zilizopo ni Mil 4.7 na kupelekea upungufu wa lita Mil 4.9 za maji ambazo huenda zikapungua zaidi baada ya mradi wa bil. 42 kuanza kutekelezwa.
Amesema kuwa mradi huo wa maji unaogharimu jumla ya bil. 42 tayari mkandarasi yupo eneo la kazi kwa ajili ya kuanza kazi, na atatekeleza mradi katika Miji sita Makambako, Njombe, Wang’ing’ombe, Rujewa,Chunya na Ifakara na kila Mji ataweka wakandarasi wadogo hivyo kupitia mradi huo vijana wengi watanufaika na ajira,kwani moja ya masharti ya utekelezaji wa mradi wafanyakazi watoke katika maeneo ambayo mradi upo hivyo vijana wa Makambako wengi watapata ajira kuanzia kazi ya ulinzi, uchimbaji mitaro, ufundi na kazi zingine kwani mkandarasi anatarajia kuweka kambi kubwa hapa Makambako.
Ameongeza kuwa licha ya fedha hizo pia Mamlaka kupitia mapato ya ndani jumla ya shilingi Mil 400 zimetengwa na jumla ya shilingi Mil 600 zimepokelewa kutoka Serikali kuu na kupelekea jumla ya bil. 1 kwa mwaka huu wa fedha kwa ajili ya mradi wa maji.
Ziara ya Mbunge leo imefanyika katika Mtaa wa Lyamkena,Kiumba Na Ikwete ikijumuisha wananchi wa Mitaa hiyo pamoja na mtaa wa Ilangamoto, Muungano,makatani na Mapinduzi ya Kijani.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa