Na. Lina Sanga
Kamati ya Fedha na Uongozi ya Halmashauri ya Mji Makambako leo imefanya ziara katika Kituo cha afya Makambako,na kutembelea duka la dawa lililopo katika kituo hicho na kukagua nyaraka mbalimbali za mauzo ya dawa pamoja na kusikiliza changamoto zinazojitokeza katika uendeshaji wa duka hilo.
Baada ya kupokea taarifa za duka hilo iliyowasilishwa na Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Makambako, Dkt. Ally Senga Wahe. Madiwani wameridhishwa na mwenendo wa biashara ya dawa katika duka hilo,na kuupongea uongozi wa Kituo hicho kwa usimamizi bora.
Dkt. Senga amesema kuwa,uamuzi wa kuanzisha mradi wa duka la dawa kituoni hapo ulitokana na kukosekana kwa baadhi ya dawa kituoni hapo ambazo hutolewa kwenye hospitali,hali iliyowalazimu wagonjwa kununua dawa maduka ya nje kwa gharama kubwa,lakini pia kwa wagonjwa waliofika usiku wa manane walipata shida ya kutafuta dawa nje na kuhatarisha maisha yao.
Mwenyekiti wa Kamati ya fedha na uongozi,Mhe. Hanana Mfikwa pamoja na wajumbe wa kamati hiyo wametoa ushauri kwa Uongozi wa kituo cha afya Makambako,Mfamasia na watumishi wanaohusika na uuzaji wa dawa katika duka hilo, kuweka kumbukumbu sahihi za takwimu za dawa zinazoingia na kutoka katika duka hilo , kwa kuandika katika daftari badala ya kutegemea mfumo pekee ili hata changamoto za kimfumo zitakapotokea takwimu ziwe salama.
Aidha,wametoa rai kwa Uongozi wa kituo hicho kuteua watumishi wachache ambao watakuwa na jukumu la kutoa huduma katika duka hilo pamoja na kulisimamia,ili kuepuka upotevu wa dawa na endapo hasara yoyote itajitokeza wawajibika kufidia.
Pia, Mhe. Hanana ametoa wito kwa Uongozi wa kituo hicho kuendelea kutoa elimu kwa wananchi, juu ya utendaji kazi wa duka hilo pamoja na umuhimu wake ili kuwajengea wananchi uelewa.
Dkt. Senga kwa niaba ya Uongozi wote wa kituo cha afya Makambako ametoa shukrani kwa pongezi za Wajumbe wa Kamati ya Fedha na Uongozi na kuahidi kufanyia kazi maoni na ushauri uliotolewa,ikiwa ni pamoja na kufanya ukaguzi wa dawa kila mwezi pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu utendaji kazi wa duka hilo.
Duka la dawa la kituo cha afya Makambako linatoa huduma kama maduka mengine ya dawa yaliyopo mitaani,kwa kuuza dawa kwa bei nafuu kwa wagonjwa waliofika kupata huduma katika kituo hicho na wagonjwa wengine ambao wapo majumbani wenye uhitaji wa dawa wenye cheti cha daktari.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa