Kamati ya Fedha na Uongozi imeziagiza kamati za ujenzi kuthaminisha nguvu za wananchi zinazotumika katika utekelezaji wa miradi ya Maendeleo na kuziainisha kwenye taarifa za miradi ili kupata gharama halisi ya mradi.
Agizo hilo limetolewa leo katika ziara ya ukaguzi,usimamizi na ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kipindi cha robo ya kwanza kwa mwaka wa fedha 2022/2023,katika Kata ya Makambako,Utengule na Kitisi katika Halmashauri ya Mji Makambako.
Akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Ikelu,Kamati ya Ujenzi ya Shule ya Sekondari Mtimbwe na Kamati ya ujenzi ya Shule ya Msingi Magongo,Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Uongozi, Mhe. Hanana Mfikwa amesema kuwa,sababu kuu ya baadhi ya miradi inayotekelezwa kwa fedha kutoka Serikali Kuu kushindwa kukamilika kwa fedha zilizoletwa ni kukosekana kwa thamani ya nguvu za wananchi kulingana na soko.
“Miradi inajengwa kwa nguvu za wananchi na fedha kutoka Serikali kuu,gharama za nguvu za wananchi hazihesabiki siku nyingine unapewa fedha zile zile ujenge bila nguvu za wananchi unashindwa kukamilisha mradi, kila siku tunasikia kwenye redio Njombe wamejenga kwa Mil.50 Iringa wamejenga kwa Mil 20 hawakuandika nguvu za wananchi,wakiletewa fedha hizo hizo bila nguvu za wananchi wanashindwa wanaambiwa wameiba kumbe gharama ya mradi haikuwa halisi”,alisema Mhe. Hanana.
Ametoa rai kwa watendaji wote na wasimamizi wa miradi pamoja na watunza stoo kuandika kila kitu kinachofanyika kwenye mradi,ikiwa ni pamoja na taarifa ya mapokezi ya vifaa vilivyonunuliwa kwa fedha za Serikali kuu au wananchi,kwa kuonyesha mchanganuo wa gharama halisi za vifaa na kazi zilizofanywa na wananchi kwa thamani ya pesa.
Aidha Kamati ya Fedha na Uongozi imeipongeza Kamati ya Ujenzi ya Shule ya Sekondari ya Kitisi na Uongozi wa Kata ya Kitisi,kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa miundombinu ya madarasa na maabara.
Kamati ya Fedha na Uongozi leo imekagua miradi mitano ya ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Ikelu,Ujenzi wa bweni shule ya Sekondari ya Mtimbwe,Mnada katika Kijiji cha Utengule,Ujenzi wa madarasa matatu na vyoo shule ya Msingi Magongo na ujenzi wa jengo la utawala,Maabara tatu,madarasa nane,ofisi mbili na choo matundu kumi katika Shule ya Sekondari Kitisi.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa