Na. Lina Sanga
Kamati ya Fedha na Uongozi ya Halmashauri ya Mji Makambako, imeridhishwa na utekelezaji wa mradi wa ufugaji wa ng'ombe wa maziwa,unaotekelezwa na kikundi cha wanawake cha Tupende Chetu kilichopo Mtaa wa Sigrid katika Kata ya Kivavi ambacho ni moja kati ya Vikundi vilivyonufaika na mkopo wa asilimia 10,unaotolewa na Halmashauri kwa vikundi vya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu.
Akizungumza na wana kikundi hao leo mara baada ya ukaguzi wa mradi huo katika ziara ya Kamati hiyo ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo,Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Makambako,Mhe. Rosemary Lwiva amesema kuwa ni nadra sana vikundi kufanya mradi kwa pamoja lakini Kikundi cha Kipende chetu kimefanikiwa kufanya ufugaji wa pamoja katika eneo moja bila kugawana mifugo na kuwapongeza kwa kuaminiana na kufanikisha mradi huo.
Ametoa wito kwa wanakikundi hao kufanya marejesho kwa wakati ili kujiongezea nafasi ya kupata mkopo mkubwa zaidi na kuwataka kuendelea kukopa hata kama mikopo ya vikundi vya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu kuhamishiwa benki kama alivyosema Mhe. Samia Suluhu Hassan,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wanakikundi hao kwa pamoja wametoa shukrani kwa Rais Samia,Mbunge wa jimbo la Makambako Mhe. Deo K. Sanga pamoja na baraza la madiwani na Mkurugenzi kwa kutoa fedha za mikopo 10% ambayo imewawezesha kununua ng'ombe na kuwapa manufaa.
Kikundi cha Tupende chetu chenye jumla ya wanakikundi watano kilipata mkopo wenye jumla ya mil. 12 na kufanikiwa kununua ng'ombe wa maziwa watatu ambao kwa sasa wameanza kukamua maziwa kwa siku wanapata lita 15 ambazo wanauza lita 1 shilingi 1,200.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa