Na. Lina Sanga
Kamati ya Fedha na Uongozi ya Halmashauri ya Mji Makambako jana imezindua zoezi la upandaji wa miti ya parachichi shuleni ,kwa kupanda miti ya parachichi shule ya Sekondari Makambako,kwa lengo la kuboresha lishe ya wanafunzi,kukuza uchumi wa shule na kujenga dhana ya kujitegemea.
Akizungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari Makambako pamoja na Walimu wa shule zote za Msingi na Sekondari za Serikali na binafsi waliohudhuria uzinduzi wa zoezi la upandaji wa miti ya parachichi shuleni,uliofanyika jana katika shule ya Sekondari ya Makambako,Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Makambako,Mhe. Hanana Mfikwa amesema kuwa ndani ya parachichi lishe,uchumi na mambo mengine yanapatikana kwani bila lishe hakuna mwanafunzi atayeweza kusoma vizuri.
Amesema kuwa,miti ya parachichi itayopandwa kila shule italeta manufaa kwa wanafunzi na shule kwani zao hilo kwa sasa linauhitaji mkubwa katika soko la dunia, lakini pia wanafunzi wanaweza kutumia tunda hilo kwenye chakula kwa muda mrefu endapo itahudumiwa vizuri.
Ameongeza kuwa,Halmashauri imeamua kupanda parachichi shuleni ili kutoa elimu kwa wanafunzi na kuwawezesha kupata ujuzi wa kilimo cha parachichi,ili baada ya kuhitimu masomo na wakati wa likizo waweze kupanda miti ya parachichi nyumbani kwao ambayo itawapa ajira na kipato cha muda mrefu baada ya miaka 3 hadi 5.
Ametoa wito kwa walimu kupanda miti waliyokabidhiwa kabla ya msimu wa mfua kuisha na kuwagawia miti ya kuihudumia wanafunzi na kila mwanafunzi ahakikishe anauhudumia mti huo kwa kumwagilia maji kadri inavyohitajika.
Naye Kenneth Haule,Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Makambako ametoa rai kwa walimu na wanafunzi kujitoa kwa ajili ya utekelezaji wa kilimo cha parachichi katika shule zao,kwa kutumia rasilimali zinazopatikana katika maeneo yao badala ya kuibua changamoto zisizo na msingi ili kukwamisha zoezi hilo kama vile ukosefu wa maji ya kutosha shuleni na samadi.
Amesema kuwa, ipo haja kwa jamii kuondoa dhana ya kuwatumikisha wanafunzi katika utendaji wa kazi za miradi mbalimbali inayoanzishwa shuleni,na kujenga dhana ya kujitegemea kwa wanafunzi kushiriki shughuli mbalimbali za miradi ya shule kwa kubeba kidumu cha maji kwa ajili ya kumwagilia mbogamboga na miti ya matunda ilyopo shule pamoja na kumjengea mtoto uwezo wa kufanya shughuli ndogondogo na kuongeza ujuzi.
Halmashauri ya Mji Makambako imetoa jumla ya miche 5,901 yenye thamani ya mil. 17.7 kwa shule zote zilizopo Katika Halmashauri ya Mji Makambako,kulingana na ukubwa wa eneo la shule, ambapo shule zenye maeneo makubwa zimepewa miche kuanzia 50 hadi 200.
Kauli mbiu ya zoezi la upandaji wa miti ya parachichi katika shule za msingi na sekondari,katika Halmashauri ya Mji Makambako inasema” BORESHA LISHE,KUZA UCHUMI WA SHULE,JENGA DHANA YA KUJITEGEMEA”.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa