Na. Lina Sanga
Kamishina wa ardhi Msaidizi Mkoa wa Njombe,Fulgence Kanuti amewapongeza wana ndoa wanaomiliki ardhi kwa pamoja,kwani ni nadra sana kushuhudia mume na mke kuandikisha umiliki ardhi wa pamoja.
Kanuti ametoa pongezi hizo katika mkutano wa uzinduzi wa utoaji hatimiliki kwa wananchi wa mtaa wa Sekondari,uliofanyika leo Maguvani kijiweni.
Amesema kuwa,katika Mtaa wa sekondari wana ndoa wengi wamejitokeza na kujiandikisha kama wamiliki wa pamoja wa viwanja,hali inayodhihirisha kuwa elimu ya haki ya umiliki wa rasilimali kwa mume na mke imeeleweka vema.
Kanuti amesema kuwa kupitia urasimishaji inasaidia kupata uhakika wa mipaka ya ardhi na kusaidia kupunguza migogoro ya ardhi,usalama wa miliki ya ardhi pamoja na kutambuliwa na taasisi za kifedha.
Amesema kuwa zoezi la utoaji wa hati kwa wananchi waliolipia na wanaoendelea kulipia litaendelea kwa muda ili kuwawezesha wananchi wote waliopima viwanja vyao kupitia MKURABITA kupata hati za viwanja vyao.
Naye Afisa Mipangomiji wa Mkoa wa Njombe,Anna Macha ametoa wito kwa wananchi waliopimiwa viwanja kutunza mawe ya upimaji,yaliyowekwa kwenye viwanja vyao kwani ni nyara za Serikali na zimewekwa kwa ajili ya kutofautisha wamiliki wa viwanja na kuondoa migogoro na endapo mgogoro ukitokea mawe hayo yatatumika kutatua mgogoro huo.
Pia, amewataka wananchi waliotoa maeneo yao kwa ajili ya miundombinu ya barabara,kutoa ushirikiano wa kufungua barabara zilizotolewa ili urasimishaji uwe na tija.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa