Na. Lina Sanga
Kikundi cha Vijana cha By Nature tech kutoka katika Mtaa wa Mlando, Kata ya Mjimwema katika Halmashauri ya Mji Makambako, kinachojishughulisha na kazi ya uchomeleaji vyuma kimekabidhiwa mashine tatu za kuchomelea na mashine tatu za kukatia vyuma,zilizotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana Ajira na Wenye ulemavu kupitia Ofisi ya Rais - TAMISEMI ikiwa ni sehemu ya kuwawezesha vijana kujiajiri.
Akitoa taarifa ya mapokezi ya vifaa hivyo katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Mji Makambako, Mkuu wa idara ya maendeleo ya jamii, Bi. Zuena Ungele amesema kuwa Ofisi ya Rais – TAMISEMI ilitoa maelekezo juu ya kutuma taarifa za vikundi vinavyofanya shughuli za uchomeleaji, kikundi cha By nature tech ni moja ya kati ya vikundi vilivyochaguliwa kuwa mnufaika wa mashine hizo zilizotolewa na Ofisi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana,Ajira na Wenye ulemavu kwa Halmashauri zote nchini.
Amesema kuwa, kikundi hicho chenye jumla ya vijana watano kilianzishwa mwaka 2021 na walipata mkopo wa mil 5 inayotolewa na Halmashauri kwa vikundi vya Wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu na kimefanikiwa kurejesha jumla ya shilingi mil 4.6 ndani ya muda na mnamo novemba 30,mwaka huu wanakamilisha deni lote.
Kabla ya kukabidhi mashine hizo,Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Makambako, Mhe. Hanana Mfikwa ameishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana,Ajira na Wenye ulemavu na Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa kutoa mashine hizo ili kuwawezesha vijana kujiajiri.
Amewapongeza vijana hao kwa kujitambua na kuweza kufanya marejesho ya mkopo vizuri na kuwataka kuendelea kutumia fedha wanazozipata kwa malengo,na kujiepusha na matumizi mabaya ya fedha wanazozipata kwa kufuata vipaumbele walivyojiwekea kufikia malengo yao.
Ametoa wito kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Makambako kukitumia kikundi hicho katika kazi mbalimbali za uchomeleaji katika miradi inayotekelezwa na Halmashauri,ili kukiwezesha kikundi hicho kupata fedha na kuwataka vijana kuwa wabunifu na kufanya kazi zilizo ndani ya uwezo wao badala ya kazi za kufikirika.
Elichalido Ng’olo mmoja kati ya vijana watano wanaounda kikundi cha By nature tech, amemshukuru Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan,Makamu wa Rais,Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana,Ajira na Wenye ulemavu na Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa kuwapa mashine za uchomeleaji ambazo zitawasaidia kufanya kazi kwa uhakika kwani vifaa vya zamani vimechakaa.
Ametoa hamasa kwa vijana kuunda vikundi na kuaminiana ili waweze kupata mikopo kutoka Halmashauri, na kutumia fedha hizo kufanikisha malengo waliyojiwekea kwani fedha za mikopo ya Halmashauri zipo.
Mashine walizokabidhiwa Vijana wa kikundi cha by nature tech.
Vijana wanaounda kikundi cha by nature tech.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa