Na. Lina Sanga
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Mji Makambako limeazimia ujenzi wa soko la nyanya katika Kata ya Mjimwema kuruhusu wananchi wote wenye nia ya kujenga vibanda katika soko hilo kupewa eneo na kusainishwa mkataba wa ujenzi,kwani wadau waliokuwa wakifanya biashara katika soko hilo wameonyesha kushindwa kukamilisha ujenzi ndani ya muda uliopangwa na wengine kutojitokeza kabisa.
Azimio hilo limetolewa leo katika mkutano wa baraza la Madiwani katika kipindi cha kuishia robo ya kwanza (julai – septemba)katika mwaka wa fedha 2023/2024 mara baada ya diwani wa Kata ya Mjimwema,Mhe. Nolasko Mlowe kuhoji hatima ya ujenzi wa soko hilo kutokana na ujenzi kusimama kwa muda mrefu.
Mhe. Hanana Mfikwa, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Makambako ambaye ndiye Mwenyekiti wa baraza la Mdiwani amesema kuwa,suala la ujenzi wa soko la nyanya limechukua muda mrefu ,hivyo kwa sasa ni wakati wa kila mwananchi kutangaziwa kuhusu fursa ya ujenzi wa vibanda katika soko hilo kwani wadau ambao walikuwa wakifanya biashara katika soko hilo wameonyesha wazi kuwa hawawezi kujenga.
Ametoa wito kwa wananchi wote wenye nia ya kujenga vibanda kwenye soko hilo ndani ya muda uliopangwa,kufika katika ofisi ya Mkurugenzi ili wapewe utaratibu na kusaini mkataba wa ujenzi ili Halmashauri ipate mapato na wananchi wapate huduma.
“Mheshimiwa diwani wa eneo husika kawaelimishe watu wako kwamba sisi Halmashauri tumengojea kwa muda wa kutosha, mtu yeyote ambaye hata kuwa na uwezo au nia ya kujenga,sisi tunampatia mtu mwingine tusiwe na lawama yoyote,zaidi ya miaka mitano tunaongea kitu kama hicho ni watu wa ajabu hatuwezi tukafika kwa namna hiyo ,lazima kitu chochote kiwe na mpaka wa muda ,hivyo yeyote anayetaka kujenga vibanda afike kwa Mkurugenzi apewe mkataba na apewe eneo ajenge vibanda ndani ya muda unaotakiwa na hakutakuwa na nyongeza za hovyo hovyo katika mikataba ya namna hiyo,habari ya tumenyang’anywa vibanda wamepewa matajiri tumewatangazia na tumevumilia kwa muda mrefu,vibanda anajenga mtu yeyote bila kuathiri mikataba”,alisema Mhe. Hanana.
Awali akijibu hoja hiyo, Bi. Appia Mayemba,Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Makambako amesema kuwa,zoezi la ujenzi wa soko la nyanya lilitangazwa ,kipaumbele ilikuwa wadau waliokuwa wanafanya biashara katika soko hilo na walipatikana wadau ishirini na kuna ujenzi wa vibanda 20 utaendelea baada ya kuongezewa mkataba mpya na kwa sasa kila mwananchi anaruhusiwa kujenga kwa kufuata utaratibu uliowekwa kwani wadau waliokuwa sokoni hapo hawaonyeshi ushirikiano.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa