Na. Lina Sanga
Mhe Ummy Mwalimu,Waziri wa Afya amewahakikishia wakazi wa Mkoa wa Njombe kuwa hakuna kilichosimama katika ujenzi wa kiwanda cha mipira ya mikono cha MSD kilichopo Mtaa wa Idofi katika Halmashauri ya Mji Makambako.
Ametoa kauli hiyo leo katika ziara yake katika kiwanda hicho mara baada ya Mbunge wa jimbo la Makambako, Mhe. Deo Sanga kuhoji kuhusu ukamilishaji wa kiwanda hicho na aina ya bidhaa zitazozalishwa mbali na uzalishaji wa mipira ya mikono (gloves).
Mhe. Ummy amesema kuwa,chini ya Serikali ya awamu ya sita ya hakuna kilichosimama kwani ujenzi wa kiwanda hicho bado unaendelea na kwa mwaka huu kuna maendeleo makubwa ya mradi huo na Serikali kwa sasa imetoa Bil. 11 na itaendelea kutoa fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa miradi ya maendeleo yote iliyoanzishwa katika Serikali ya awamu ya tano.
Pia,katika sekta ya Afya wamedhamiria kuongeza uzalishaji wa ndani wa dawa,vifaa tiba na bidhaa nyingine za Afya ili kupunguza uhaba wa dawa na vifaa tiba, kwani kwa sasa bidhaa hizo asilimia 85 zinaagizwa nje kwa gharama kubwa na zinafika kwa kuchelewa nchini hivyo kusababisha uhaba wa dawa na vifaa tiba.
Amesema kuwa, lengo la Serikali kujenga viwanda vya dawa na vifaa tiba nchini ni kufikia asilimia 50 ya bidhaa za Afya kununuliwa ndani ya nchi ifikapo 2030 kupitia Bohari kuu ya dawa (MSD) ambapo kwa sasa ni asilimia 15 pekee za bidhaa za Afya zinanunuliwa ndani ya nchi.
Ameongeza kuwa ,kwa sasa kuna jumla ya viwanda 30 vya dawa na vifaa tiba na viwanda 11 vinafanya kazi ikiwa ni pamoja na viwanda viwili vya uzalishaji chupa Mil. 90 za maji tiba (dripu) na mahitaji ni Mil 24 hadi 26 ,hivyo maji tiba hayatanunuliwa tena nje bali yataanza kununuliwa nchini.
Amebainisha kuwa,Bohari ya dawa (MSD) katika bajeti ya mwaka 2021/2022 imenunua bidhaa za Afya zilizotengenezwa ndani ya nchi zenye thamani ya Bil 14. 1,bajeti ya mwaka 2022/2023 imenunua bidhaa za Afya zenye thamani ya Bil. 39.4 matarajio kwa sasa ni kuhakikisha ununuzi wa bidhaa hizo kufikia Bil. 50 ifikapo kipindi cha kufunga mwaka wa fedha wa Bunge.
Ametoa rai kwa Mbunge wa jimbo la Makambako kuridhia kiwanda hicho kuanza na uzalishaji wa mipira ya mikono kwa sasa na mapendekezo ya Kamati iliyopita katika kiwanda hicho yatajadiliwa katika kikao cha pamoja cha kamati za Bunge za uwekezaji mitaji ya Umma, Afya na masuala ya UKIMWI, Hesabu za Serikali na Mbunge wa jimbo la Makambako.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa