Na. Lina Sanga
Taarifa hiyo imetolewa na Waziri wa Kilimo,Mhe. Hussein Bashe katika kikao cha wadau wa kilimo kilichofanyika jana katika Halmashauri ya Mji Makambako,na kubainisha kuwa kiwanda hicho kitakuwa mahususi kwa ajili ya parachichi ambazo zitakataliwa kiwandani kwa kukosa ubora wa kuuzwa katika soko la dunia.
Mh. Bashe amesema kuwa ,Serikali inafanya mazungumzo na kampuni binafsi moja na wasipofikia muafaka Serikali itaweka fedha kwa ajili ya kuwekeza kiwanda hicho ili kumuokoa mkulima asipoteze tunda lolote.
“Tumemwambia huyo mwekezaji lete mashine utafunga katika eneo la Serikali na tutakupa mkataba wa miaka mingi,nimeshaongea nae na kwa sasa atawasiliana na Mkoa na mamlaka zinazohusika na eneo lililopendekezwa,ili parachichi za wakulima zisitupwe ambazo hazifai kusafirishwa nje zipelekwe kiwandani kwa ajili ya kuchakata mafuta,safari hii itatuchukua Muda hivyo ni lazima tuianze sasa”,alisema Mhe. Bashe.
Aidha,Mhe. Bashe amebainisha kuwa,Serikali itabadilisha bei ya zao la chai kwa mkulima ambayo inauzwa bei ndogo tofauti na bei ya sokoni,Wizara imefanya utafiti wa mzunguko wa bei ya chai kutoka Tanzania na ubora wake na kupata suluhisho la bei ya mkulima kuuza chai na bei mpya itatangazwa baada ya Mkutano wa wadau wa kilimo cha chai utakaofanyika leo januari 18,Mkoani Iringa.
Pia amebainisha kuwa,mchakato wa kuanzishwa kwa mnada wa zao la chai nchini umekamilika na gharama za usafirishaji wa kontena moja la chai kutoka Njombe hadi Mombasa ni Mil. 8.2 na gharama ya kutoka Njombe hadi Dar es salaam ni Mil. 3.9 kwa kontena moja hivyo kuanzishwa kwa mnada wa chai katika Mkoa wa Dar es salaam hakutakuwa na sababu ya kupeleka chai Mombasa kwani mnada huo hauna tozo yoyote Serikali inabeba gharama zote.
Amesema kuwa,lengo la kuanzishwa kwa mnada huo ni kupata uwazi wa bei ya chai ili kupata uwiano wa bei ya chai anayouza mkulima na bei ya chai ambayo mfanyabiashara anauza katika soko la dunia.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa