Na. Lina Sanga
Iringa
Mikoa mitatu ya Nyanda za juu Kusini imeanza mafunzo ya Mradi wa BOOST leo yanayotolewa na Ofisi ya Rais –TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia Mkoani Iringa.
Akifungua mafunzo hayo Mkurugenzi wa michezo Ofisi ya Rais –TAMISEMI, Yusuph Singo ambaye pia ni mratibu wa mafunzo hayo amesema kuwa,mradi wa BOOST ni mradi wa kuimarisha ujifunzaji shule za awali na msingi unaofadhiliwa na benki ya dunia na unatarajiwa kutumia jumla ya trillion 1.15.
Amesema kuwa kupitia fedha hizo jumla ya madarasa 12,000 yanatarajiwa kujengwa katika shule za awali na msingi kwa miaka mitano ambapo kwa mwaka mmoja jumla ya madarasa 3,000 yatajengwa,kufunga vifaa vya TEHAMA kwenye vituo vya walimu na shule za msingi 800 na utekelezaji wa mradi huo umeanza mwaka huu 2022/2023 na unatarajiwa kumalizika 2025/2026 kwa utaratibu wa lipa kulingana na matokeo.
Ameongeza kuwa mradi wa BOOST una jumla ya afua 8 za utekelezaji ikiwa ni pamoja na afua ya Mamlaka za Serikali za Mitaa kutekeleza mafunzo endelevu ya walimu kazini,Upatikanaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia,Kuongeza uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la awali,Mpango wa shule salama kwa shule 6,000 na Mpango wa ujenzi wa miundombinu ya madarasa na vyoo.
Ametoa wito kwa timu za utekelezaji wa mradi huo ngazi za Mikoa na Halmashauri kuhakikisha wanasimamia miradi kwa kuzingatia ubora na viwango vinavyokubalika,kwani endapo utekelezaji wa miradi hiyo utakuwa hauridhishi fedha za utekelezaji hazitatolewa.
Mikoa ya Nyanda za juu Kusini iliyoshiriki mafunzo hayo yaliyoanza kutolewa leo na yatahitimishwa kesho ni Mkoa wa Iringa,Njombe na Ruvuma kwa kuhusishwa washiriki 250 kutoka ngazi za Mikoa na Halmashauri.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa