Na. Lina Sanga
Makamu wa Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Dkt Philip Mpango ameuagiza uongozi wa Bohari ya Dawa nchini (MSD),kuhakikisha shughuli za uzalishaji katika kiwanda cha kutengeneza mipira ya mikono(gloves) kilichopo Mtaa wa Idofi,katika Halmashauri ya Mji Makambako unaanza kufanyika januari mosi,2024.
Dkt. Mpango ametoa agizo hilo leo mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika kiwanda hicho,na kuagiza uongozi wa kiwanda hicho pamoja na Wizara ya Afya kuandaa taarifa ya kina inayoeleza sababu ya kutofungwa kwa mitambo iliyopo kiwandani hapo kwa miaka miwili pamoja na hoja za Mkaguzi mkuu wa Serikali (CAG).
Amesema kuwa changamoto za kiutendaji zilizopo katika kiwanda hicho zishughulikiwe na kuwahakikishia wakazi wa Idofi kuwa kiwanda hicho hakitahamishwa kitaendelea kuwa Idofi na kuzalisha dawa,vifaa tiba na vitendanishi.
Amemuagiza Naibu Waziri wa Wizara ya Afya na Naibu Waziri wa ofisi ya Rais TAMISEMI, kuhakikisha bidhaa zingine zinazalishwa katika kiwanda hicho kwa kutumia miundombinu iliyopo kiwandani hapo kama maji tiba na vitendanishi vya maabara ili kuongeza tija.
Aidha,ameitaka kampuni tanzu ya MSD kuzingatia misingi ya kibiashara,ili waweze kujitegemea katika uzalishaji kutoka katika kiwanda cha Idofi na viwanda vingine na kuagiza uongozi wa kiwanda cha Idofi kuongeza ajira za wananchi wa Idofi katika kiwanda hicho hasa wanawake.
Ameagiza Wakala wa barabara Mijini na Vijijini (TARURA) kufanya tathmini ya ujenzi wa barabara ya lami kuelekea eneo la kiwanda inayokadiriwa kugharimu Bil. 1.4 na kuifikisha ofisi ya Rais TAMISEMI kwa ajili ya kupata fedha ya utekelezaji wa ujenzi huo.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa