Na. Lina Sanga
Watendaji wa halmashauri wametakiwa kuwasilisha orodha za wadaiwa wa mikopo ya asilimia kumi ya vikundi vya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu inayokopeshwa na halmashauri,ikionyesha tarehe za mikopo,muda wa deni na kata wanazotoka wadaiwa hao na kuziwasilisha kwa Katibu Tawala wa Mkoa ili kuongeza msukumo wa kukusanya madeni hayo.
Agizo hilo limetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Njombe ,Mhe.Waziri Kindamba katika mkutano maalumu wa baraza la Madiwani la kuwasilish mpango kazi na majibu ya Menejimenti kwa ajili ya utekelezaji wa hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa hesabu za Serikali kuishia Juni 30,2021.
Mhe.Kindamba amesema kuwa katika hoja ambazo hazijafungwa na zinatakiwa kufanyiwa kazi na mamlaka nyingine na hoja ambazo zimefungwa,halmashauri ya Mji Makambako imefanya vizuri sana katika kupunguza au kumaliza hoja hizo na jitihada hizo ziendelee hasa katika ukusanyaji wa deni la mikopo ya wanawake ,vijana na watu wenye ulemavu,kwa kutumia mbinu za kibenki katika utoaji mikopo hiyo na kuweka mikakati madhubuti kuhakikisha madeni yote yanalipwa kwa wakati uliopangwa.
“Sisi waswahili utamaduni wa kulipa madeni haujalimwa vizuri ndani yetu na mtu akipata fedha za namna hii anaona ni haki yake,hajui kama anawajibika kuzirudisha ili wengine waweze kukopeshwa,kila mtu ana mikakati ya namna ya kuhakikisha madeni yanalipwa wenzetu wa benki wana mikakati mizuri sana katika kuhakikisha madeni yanalipwa kwa wakati uliopangwa kama ni ndani ya siku thelathini,mkopo ukianza kwenda siku sitini mkopo unaenda kwenye matata na ukifika siku tisini unakua ni matata zaidi”,alisema Kindamba.
Amemtaka Mkurugenzi kupanga watu kwenye vitengo vya mikopo kwani waswahili kukopa harusi kulipa matanga,hivyo katika vitengo hivyo watu wa kukopesha na watu wa kudai madeni ni muhimu sana na itasaidia katika kusimamia urejeshwaji wa madeni kwa wakati,kwani kudai pia inategemea ujuzi wa mtu katika kudai pasipo kuwa na huruma.
Aidha Mhe. Kindamba amesema elimu ya fedha ni muhimu kwa vikundi hivyo ili kuwaelimisha namna ya kutumia fedha hizo katika malengo yaliyokusudia,kwani wengine hawana elimu ya mikopo wakipata mikopo wanaitumia katika malengo mengine kama kuoa na matumizi mengine.
Ametoa wito kwa Mkurugenzi wa halmashauri ya Mji Makambako kuwakabidhi Madiwani katika ufuatiliaji wa vikundi vya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu na kuhakikisha madeni yanalipwa,katika usimamizi na ukusanyaji wa mapato kwani Mji wa Makambako ni kituo cha biashara hivyo makusanyo ya mapato yaendane na hadhi ya Mji.
Pia ametoa wito kwa wananchi wote kujiandaa kushiriki zoezi la Sensa ya watu na makazi kikamilifu itayofanyika Agosti 23,2022 kwa maendeleo endelevu ya Taifa letu pamoja na kujitokeza kupata Chanjo ya Uviko 19.
Mwisho ametoa pongezi kwa halmashauri ya Mji Makambako kwa kupata hati safi ya ufungaji wa hesabu za Serikali,usimamizi wa utekelezaji wa maelekezo yanayotolewa na Serikali,utekelezaji wa Miradi,Utoaji wa huduma kwa wananchi pamoja na kusimamia miongozo mbalimbali iliyowekwa, pamoja na ukamilishaji wa zoezi la anwani za makazi na postikodi kwa kutekeleza zoezi hilo ndani ya muda na kukamilisha kwa asilimia mia moja.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa