Na. Lina Sanga
Halmashauri ya Mji Makambako kupitia mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha 2021/2022 imenunua pikipiki 10, zenye thamani ya Mil 29.5 kwa ajili ya kuwawezesha watumishi Kutekeleza majukumu yao kwa wakati na kuwafikia wananchi Wanaohitaji huduma bila kikwazo.
Akikabidhi pikipiki hizo leo,Mhe. Hanana Mfikwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Makambako amempongeza Mkurugenzi,timu ya wataalamu na madiwani,kwa kuridhia Ununuzi wa pikipiki hizo ili kutatua changamoto ya usafiri kwa watumishi hasa watendaji wa Kata za pembezoni mwa Mji.
Aidha amewapongeza wananchi wa Halmashauri ya Mji Makambako kwa kuchangia mapato ya Halmashauri ambayo yanawezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali,ikiwa ni pamoja na ununuzi wa vyombo vya usafiri ambavyo vinatumika kutoa huduma kwa wananchi ambao ni walipaji wazuri wa kodi na ushuru mbalimbali za Halmashauri.
Ametoa wito kwa watumishi waliokabidhiwa pikipiki hizo,kuzingatia sheria za usalama barabarani na kutumia pikipiki kwa kazi zilizokusudiwa pamoja na kuzitunza.
Jumla ya watendaji wa Kata watano wamekabidhiwa Pikipiki leo ili kuwawezesha kuwahudumia wananchi bila Kikwazo cha usafiri,Kata zilizopata pikipiki ni pamoja na Kata ya Mlowa, Kitandililo, Mahongole, Utengule na Msimamizi Wa Watendaji.
Pia Wahasibu wa Mapato wawili wa Kitengo cha fedha wamekabidhiwa Pikipiki ili waweze kuongeza nguvu katika usimamizi na ukusanyaji wa mapato, Afisa biashara mmoja kwa ajili ya kufuatilia masuala mbalimbali ya biashara,uwekezaji na Viwanda ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji wa leseni za biashara.
Lakini pia,Afisa maendeleo ya jamii mmoja kwa ajili ya ufuatiliaji wa Mikopo na marejesho ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa vikundi vya Wanawake,Vijana na watu wenye ulemavu pamoja na pikipiki moja kwa Afisa Mifugo kwa ajili ya ufuatiliaji wa shughuli za ufugaji wa samaki na mapato yanayotokana na Samaki pamoja na ukaguzi wa nyama.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa