-Wanufaika watakiwa kusoma na kuielewa mikataba ya mikopo kabla ya kusaini kuepuka adhabu.
Na. Lina Sanga
Mwanasheria wa Halmashauri ya Mji Makambako, Bi. Amina Kassim amewataka wanufaika wa mikopo ya asilimia 10,kusoma na kuielewa mikataba ya mikopo kabla ya kusaini ili kutokuwa na sintofahamu katika utekelezaji wa vipengele vya sheria na kanuni zinazohusu utoaji wa mikopo hiyo.
Bi. Amina ametoa wito huo leo katika mafunzo kwa wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 awamu ya pili kwa mwaka wa fedha 2024/2025, yaliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji Makambako, ili kuwajengea uelewa wanufaika hao kabla ya kuanza kutekeleza miradi waliyoombea mikopo.
Amesema kuwa, Serikali kwa kutambua umuhimu wa mikopo hiyo na changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wa miradi, imetoa nafasi kupitia sheria na kanuni za mikopo hiyo ili kuwawezesha wanufaika kugawana fedha na kuanzisha miradi binafsi,kuomba kubadilisha mradi baada ya mradi kusuasua,kuomba punguzo la kiwango cha marejesho au nyongeza ya Muda wa marejesho.
"Ili muweze kutekeleza vipengele vya sheria ya mikopo ni lazima msome na kuuelewa mkataba husika,ili muweze kutambua wajibu na haki zenu kwani kusaini mikataba bila kusoma pia ni kosa kisheria,nawasisitiza msome na kuielewa kama kuna kipengele hukielewi uliza ueleweshwe", alisema Bi. Amina.
Naye Mkuu wa divisheni ya maendeleo ya jamii katika Halmashauri ya Mji Makambako, Bi. Lilian Mwelupungwi kabla ya kufungua mafunzo hayo, aliwataka wanufaika wote kuzingatia matumizi sahihi ya mikopo hiyo pamoja na kufanya marejesho ndani ya muda husika ili kujiongezea nafasi ya kupata mkopo mkubwa zaidi.
Spailo Nzalalila, Mmoja kati ya wanufaika wa mikopo hiyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa kikundi cha Boda five ametoa rai kwa Serikali kuendelea kutoa elimu ya mikopo ya asilimia 10 kwa vijana ili waweze kuunda vikundi, na kupata mikopo itayowawezesha kutekeleza miradi ya kiuchumi kwa mikopo isiyo na riba.
Halmashauri ya Mji Makambako katika kipindi cha awamu ya pili kwa mwaka wa fedha 2024/2025 imetoa jumla ya Mil 350.8 kwa vikundi 11 vya wanawake,vikundi 17 vya vijana na watu wenye ulemavu 2.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa