Na. Lina Sanga
Serikali imetoa jumla ya Mil. 583.2 kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari Mpya katika Kijiji cha Mbugani, Kata ya Kitandililo ili kuwapunguzia mwendo wanafunzi wanaojiunga na masomo ya sekondari kutembea zaidi ya kilomita 20 kila siku kutoka Kijijini hapo hadi shule ya sekondari Mlowa na Kitandililo.
Taarifa hiyo imetolewa leo na Afisa elimu sekondari wa Halmashauri ya Mji Makambako,Mwl. Aderick Nombo wakati akiutambulisha mradi huo kwa wananchi wa Kijiji cha Mbugani ili waweze kushiriki na kuumiliki mradi.
Mwl. Nombo amesema kuwa,Mil. 583 ni nyingi zikitamkwa lakini katika utekelezaji wa miradi haitoshi ,hivyo jitihada za wananchi zinahitajika ili kupunguza gharama ili fedha hizo zikamilishe mradi na uanze kutumika.
Ametoa rai kwa wananchi wa Kijiji cha Mbugani kuendelea kujitoa kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo na kuachana na maneno ya wapinga maendeleo kuwa fedha hizo ni nyingi na kukwamisha ukamilishaji wa mradi.
Amesema kuwa,katika hatua za awali za mradi kila mwananchi ajitoe kushiriki kama kusafisha eneo, kumwaga jamvi,maji na kuchimba msingi, ili fedha zilizoletwa na Serikali zitoshe kukamilisha mradi ifikapo Oktoba 30,2023 shule hiyo isajiliwe mapema na ianze rasmi ifikapo januari,2024.
Naye, Afisa Maendeleo ya jamii wa Halmashauri ya Mji Makambako, Bi. Zuena Ungele ametoa wito kwa wananchi wa Mbugani kuupokea mradi na kushiriki katika shughuli mbalimbali,ili mradi ukamilike kwa wakati kupitia fedha zilizotolewa na Serikali kwa kuzingatia umuhimu wa shule hiyo katika Kijiji hicho na kuwalinda watoto dhidi ya ukatili ambao wanafanyiwa njiani kama kubakwa na kulawitiwa kutokana na kutembea umbali mrefu.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa