Na. Lina Sanga
Njombe
Waziri wa Maliasili na Utalii,Mhe. Balozi Pindi Chana(Mb) ,leo amezindua Mkakati wa kutangaza utalii Mikoa ya kusini mwa Tanzania,na Kuendeleza utalii wa utamaduni wa Mikoa hiyo kwani kuna utajiri mkubwa sana wa utamaduni kama ngoma, mila, desturi pamoja na vyakula ambavyo ni sehemu ya utalii.
Mhe. Chana amesema kuwa kupitia mikakati hiyo hatua mbalimbali zitazochukuliwa zimeainishwa,ili kuchochea ukuaji wa shughuli za utalii katika Mikoa ya Kusini ikiwemo Mkoa wa Iringa, Njombe, Rukwa, Katavi, Ruvuma, Mbeya, Mtwara,Lindi,Songwe na Morogoro.
Amesema kuwa,mikakati hiyo imezingatia fursa za utalii zilizopo katika Mikoa ya Kusini hususani utalii wa utamaduni ambao ni hazina kubwa kwa mikoa hiyo,kwani utalii sio tu uwepo wa wanyama bali hata utalii wa utamaduni na kwasasa kuna ubunifu wa aina mpya ya utalii ikiwamo utalii wa masuala ya nyuki,maua na matibabu.
Aidha,Mhe. Chana amesema kupitia utekelezaji wa mikakati hiyo wanatarajia utaongeza idadi ya watalii wanaotembelea ukanda wa Kusini,hivyo kuongeza ajira na fursa za uwekezaji pamoja na kuongezeka kwa kipato cha mwananchi mmoja mmoja na mapato ya Serikali kwa ujumla.
Ametoa rai kwa wadau wa utalii na wananchi wote wa Mikoa ya Kusini kuchangamkia fursa za utalii, zilizopo na zitazojitokeza ili kujipatia kipato na kuongeza Mapato ya Mikoa yao.
Pia amewaomba Wakuu wa Mikoa kuwaelekeza watumishi wanaohusika na sekta za maliasili na utalii,kushirikiana na bodi ya Utalii Tanzania katika utekelezaji wa mikakati ya utalii iliyozinduliwa.
Ametoa rai kwa viongozi na wadau wote wa utalii kuungana na Mhe. Samia Suluhu Hassan,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuendeleza programu ya Tanzania The Royal Tour pamoja,na kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii katika kuendeleza na kubuni mikakati mbalimbali na mazao mbalimbali ya masuala ya utalii.
Mwisho amewashukuru wakuu wa Mikoa kwa kutambua maeneo ya utalii katika mikoa yao na kuwataka, kuendelea kuyatambua maeneo mengine ambayo bado hayajatambulika na kutangazwa kwenye gazeti la Serikali,kama maeneo muhimu ya utalii na Wizara ya Maliasili na Utalii ipo tayari kushirikiana na Mikoa hiyo katika utambuzi wa maeneo yote ya utalii.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa