Na. Lina Sanga
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Makambako na baraza la Madiwani,Mhe. Hanana Mfikwa amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Makambako kumualika Kamishna wa ofisi ya ardhi Mkoa wa Njombe katika Mkutano wa baraza la madiwani lijalo ili ajibu hoja za wananchi kuhusu hati za viwanja kuchelewa kutolewa tofauti na awali.
Mhe. Hanana ametoa agizo hilo leo katika Mkutano wa baraza la Madiwani kwa kipindi cha kuishia robo ya kwanza kwa mwaka wa fedha 2022/2023,uliofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Mji Makambako.
Amesema kuwa ipo haja ya Kamishna wa ardhi kuhudhuria mkutano wa baraza lijalo ili atoe majibu kuhusu malalamiko ya wananchi waliopimiwa hati zao kuchelewa kutolewa ingawa ofisi ipo ndani ya Mkoa wa Njombe tofauti na nyakati za nyuma ambapo ofisi hizo zilipokuwa Mkoa wa Mbeya.
Mhe. Salum Mlumbe,diwani wa Kata ya Lyamkena amesema kuwa upatikanaji wa hati miliki za viwanja kwa sasa ni changamoto tofauti na miaka ya nyuma ambapo huduma hiyo ilikuwa ikitolewa mkoa wa Mbeya,hali inayowakwamisha wananchi kujikwamua kiuchumi kupitia hati hizo na kusababisha wananchi wengi kukosa mwamko wa kupimiwa viwanja.
Aidha Mhe. Hanana ametoa wito kwa wananchi kushiriki mikutano ya baraza la madiwani ili kusikiliza na kupata uelewa wa masuala mbalimbali yanayofanyika na yanayotarajiwa kufanyika katika Halmashauri yao.
Wakati huo huo,Mhe. Hanana ametoa rai kwa wajenzi wa vibanda na wafanyabiashara katika soko la nyanya lililopo katika Kata ya MjiMwema,kukamilisha ujenzi wa vibanda ndani ya miezi tisa waliyopewa na kwa ambaye hana uwezo wa kukamilisha ujenzi ndani ya muda huo apishe wenye uwezo wajenge.
Pia, ametoa rai kwa wananchi wote ndani na nje ya Halmashauri ya Mji Makambako kujitokeza kununua viwanja vinavyouzwa na Halmashauri,vilivyopangwa kisasa katika Mtaa wa Idofi,Kihanga na Majengo kwa ajili ya ujenzi wa makazi na uwekezaji wa viwanda vidogo vidogo na magahala.
Halmashauri ya Mji Makambako ilifanya upimaji wa jumla ya viwanja 219 kwa ukubwa na matumizi mbalimbali kama vile vinjwa vya makazi pekee vinavyouzwa shilingi 2,500 kwa mita za mraba,makazi na biashara vinauzwa shilingi 3,000 kwa mita za mraba,shule ya awali vinauzwa shilingi 3,000 kwa mita za mraba,viwanda vidogo na maghala vinauzwa shilingi 3,000 kwa mita za mraba eneo la idofi na kihanga.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa