Na. Lina Sanga
Mkuu wa wa Wilaya ya Njombe,Mhe. Kissa Gwakisa Kasongwa leo amewakabidhi Maafisa Ugani na Ushirika wa halmashauri ya Mji Makambako pikipiki 28 na amewataka Maafisa hao kuzitunza pikipiki walizokabidhiwa,ili ziweze kudumu kwa muda mrefu kwa kuzitumia kwa kazi iliyokusudiwa badala ya kubebea nyasi za ng’ombe,Mkaa na Mizigo mingine kuliko uwezo wa pikipiki hizo.
Mhe. Kasongwa ametoa wito huo wakati wa zoezi la ugawaji wa pikipiki hizo zilizotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa Maafisa Ugani wa Mikoa kumi Nchini ili kuwawezesha maafisa hao kuwafikia wakulima kwa urahisi.
Aidha Mhe. Kasongwa amesema kuwa Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa sasa ametoa pikipiki hizo kwa mikoa kumi ya mwanzo,ikiwa ni mikoa ambayo inatekeleza shughuli za kilimo na kuzalisha chakula kwa ajili ya Nchi yetu,hivyo baada ya kuwezeshwa pikipiki hizo ni matarajio ya Serikali kuona matokeo makubwa katika utendaji kazi wa maafisa Ugani.
“Mhe. Samia Suluhu Hassan anasema kazi iendelee hivyo kupitia uwezeshwaji huu wa pikipiki 28 tunaamini kazi itaendelea zaidi,kwa kupata matokeo makubwa katika sekta ya kilimo kwa kuona utofauti wa kabla ya kupewa pikipiki na baada ya kupewa pikipiki hizi,hivyo mnatakiwa kujiwekea malengo ya kabla ya kuwa na pikipiki hali ilikuaje na baada ya kupewa pikipiki”,amesema Mhe. Kasongwa.
Pia ameipongeza halmashauri ya Mji Makambako kwa kuitikia wito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa kuhusu ugawaji wa pikipiki hizo kwa Maafisa Ugani,na halmashauri ya Mji Makambako imetekeleza ugawaji wa pikipiki hizo zikiwa na usajili wa awali ili zianze kazi na mengine yataendelea kukamilishwa kwenye maeneo yao kazi.
Akitoa shukrani kwa niaba ya Maafisa Ugani wote,Bw.Patrick Kyalawa ambaye ni Afisa Kilimo wa Kijiji cha Mkolango ametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali na kuwapa pikipiki hizo ambazo zitawasaidia kuwafikia wakulima kwa wakati,na kuleta matokeo makubwa tofauti na mwanzo kwani awali ilikuwa ngumu kuwafikia wakulima kwa wakati,kwani vituo vya kazi vipo maeneo tofauti maeneo mengine kuna milima na mabonde na kuwafikia wakulima kwa haraka ilikuwa ngumu,lakini kwa sasa wataweza kuwafikia wakulima kwa wakati na kutatua changamoto kwa haraka na kuleta mabadiliko makubwa kupitia idara ya Kilimo.
Naye Afisa Usafirishaji wa halmashauri ya Mji Makambako,Bw. David Mbunda ametoa rai kwa Maafisa ugani wote waliokabidhiwa Pikipiki hizo kuzingatia sheria za barabarani na kuhakikisha wanapata leseni za udereva pamoja na kuhakikisha wanatunza pikipiki hizo na kuzitumia kwa matumizi yaliyokusudiwa na si vinginevyo.
Halmashauri ya Mji Makambako imepokea jumla ya pikipiki 28 ambapo pikipiki 27 ni kwa ajili ya Maafisa Ugani na pikipiki moja kwa ajili ya Afisa ushirika wa halmashauri ya Mji Makambako.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa