Na. Lina Sanga
Mwenge wa Uhuru 2024 umepitia Miradi 4 yenye thamani ya Mil. 308 katika Halmashauri ya Mji Makambako ambapo kati ya miradi hiyo,miradi miwili imefunguliwa na Mwenge wa Uhuru.
Akizungumza mara baada ya kutembelea mradi wa parachichi kwa wanufaika wa TASAF na kijana Sumbuko Sanga mnufaika wa Mkopo wa asilimia kumi inayokuwa ikitolewa na Halmaahauri na kabla ya kufungua mradi wa nyumba pacha ya watumishi wa Zahanati ya Kijiji cha Nyamande na madarasa matatu katika shule ya sekondari Mbugani-Kitandililo ,Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru 2024, Ndg. Godfrey Mzava amesema kuwa, utekelezaji wa miradi hiyo unaridhisha na thamani ya pesa inaonekana kama Serikali ilivyokusudia.
Aidha amewataka wanufaika wa TASAF kuzalisha miradi wanayowezeshwa na Serikali ili waweze kujitegemea kiuchumi,kwani lengo la Serikali ni kuona wanufaika wote wanapiga hatua kwa kuzalisha miradi ambayo wanawezeshwa na Serikali ikiwa ni pamoja na mradi wa parachichi.
Pia ameitaka Halmashauri ya Mji Makambako kumpa kipaumbele kijana mwenye ulemavu, Ndg. Sumbuko Sanga fundi selemala ambaye ni mnufaika wa mkopo wa asilimia kumi uliokuwa ukitolewa na Halmashauri kwa kumuwezesha kupata mashine kubwa kwa ajili ya kazi zake na kumtafutia eneo kubwa la kufanyia shughuli zake ili kumuwezesha kuwa na eneo kubwa kwa ajili ya kuhifadhia samani anazotengeneza kabla ya kuchukuliwa na mteja.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa