Na. Lina Sanga
Watendaji wa halmashauri ya Mji Makambako pamoja na Madiwani wametakiwa kuhakikisha lengo la ukusanyaji mapato katika mwaka wa fedha 2021/2022 unafikia asilimia mia moja kabla ya mwaka kuisha.
Rai hiyo imetolewa leo na Mwenyekiti wa baraza la Madiwani katika halmashauri ya mji Makambako,Mhe. Hanana Mfikwa wakati wa ufunguzi wa mkutano wa baraza la madiwani kuishia robo ya tatu kwa kipindi cha januari hadi machi kwa mwaka wa fedha 2021/2022,uliofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya mji makambako.
Mhe. Hanana amesema kuwa fedha zinazokusanywa zinaiwezesha halmashauri na Serikali kutekeleza shughuli mbalimbali kwa faida ya wananchi,hivyo ni wajibu wa kila mtendaji wa Serikali,viongozi wa wafanyabiashara na Madiwani kukusanya mapato ya halmashauri kwa haki bila kubugudhi wananchi hadi kufikia asilimia miamoja la lengo la ukusanyaji mapato.
Aidha Mhe. Hanana ameagiza usimamizi wa shughuli za ujenzi katika maeneo mbalimbali,mtendaji na diwani wana wajibu wa kusimamia na kuandika taarifa za miradi,kwa uwazi kwa kuonyesha fedha za miradi zilizotolewa na Serikali,nguvu ya wananchi na michango ya viongozi na halmashauri ili kuondoa malalamiko ya wananchi dhidi ya Serikali.
“Baadhi ya wananchi huuliza Serikali imetufanyia nini katika ujenzi wa miradi mbalimbali,hivyo endapo mtendaji ukiandika na kutafsiri taarifa ya mradi vizuri kwa kutaja fedha zilizotolewa na Serikali katika ujenzi wa mradi,mchango wa diwani na viongozi wengine,mchango wa halmashauri na nguvu za wananchi katika kukamilisha mradi itasaidia kuwabana wananchi ambao hawajashiriki katika kuchangia lakini pia watatambua kazi inayofanywa na Serikali”,alisema Mhe. Hanana.
Aidha amewataka wananchi wote kutunza mazao yao na kuweka akiba ya chakula ili kukabiliana na janga la njaa,ambalo linaweza kutokea kutokana na hali halisi iliyopo mashambani kutokana na uhaba wa mvua.
Wakati huo huo ametoa wito kwa wananchi wote kushiriki zoezi la utoaji chanjo ya Uviko 19 pamoja na polio inayotolewa kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano ili kuwalinda na ugonjwa huo unaosababisha kupooza,lakini pia kila Mwananchi ahakikishe nyumba yake ina kibao che namba na ajiandae kushiriki Sensa ya watu agosti 23,2022.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa