Na. Lina Sanga
Mkoa wa Njombe umezindua mwongozo wa elimu leo na kuweka mkakati mpya wa kutokomeza ziro kwa wanafunzi wa kidato cha nne,ambapo walimu wametakiwa kuwafundisha watoto masomo matano wanayoyaweza badala ya kumi na moja.
Akiwasilisha mkakati huo Mkuu wa Mkoa wa Njombe,Mhe. Anthony Mtaka katika uzinduzi wa Mwongozo wa elimu uliofanyika leo shule ya sekondali Mpechi, amesema kuwa badala ya walimu kuendelea kuwafundisha wanafunzi masomo yote hata ambayo hawayawezi ni wakati sasa walimu kuwapima wanafunzi hao ili kutambua masomo matano ambayo kila mwanafunzi anayaweza na kuwafundisha zaidi ili waweze kufaulu vizuri badala ya kuwaongezea mzigo wa masomo mengine ambayo hawayawezi.
Ametoa rai kwa walimu na wanafunzi kuhakikisha wanatokomeza ziro na shule ya Serikali itayofaulisha na kuingia kumi bora,itapewa milioni tano taslimu kwaajili ya walimu sio matumizi ya shule na mwanafunzi atayefaulu daraja la kwanza la pointi saba atapewa laki tano,mwanafunzi wa kike na wenye mahitaji maalumu wataopata daraja la kwanza la pointi nane na tisa (single digit) watapewa laki tano,Mwalimu atayefaulisha kila alama A atapewa elfu ishirini na alama B atapewa elfu tano.
Amesema kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa itatoa fedha hizo kama motisha kwa walimu na wanafunzi,ili mkakati wa kutokomeza ziro ufanikiwe lakini pia wazazi na walezi wa wanafunzi hao wana nafasi kubwa sana katika ufaulu wa wanafunzi hivyo ili mkakati huo ufanikiwe wazazi hawana budi kuhakikisha wanawasimamia watoto wao kujisomea.
Akielezea mikakati iliyopo katika vitabu vitatu vilivyozinduliwa leo Afisa elimu Mkoa wa Njombe,Mwl. Nelasi Mulungu amesema mikakati iliyopo katika vitabu hivyo ni kuhakikisha wanafunzi wote wanaoanza darasa la kwanza wanamaliza darasa la saba,kuhakikisha wanafunzi wote wanapofika darasa la pili wanajua kusoma,kuandika na kuhesabu na kila mwanafunzi anayeanza kidato cha kwanza anamaliza kidato cha nne.
Mulungu amesema mikakati hiyo inawaelekeza viongozi namna ya kusimamia na kufuatilia shule katika maeneo yao,huku ikiwalenga hasa Walimu wakuu,Wakuu wa shule,Maafisa elimu Kata,viongozi ngazi ya Halmashauri na Mikoa.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa