Na. Lina Sanga
Ofisi ya Rais ,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kupitia mfumo wa TAUSI imefanikiwa kuboresha utoaji wa huduma ya ukusanyaji wa kodi za majengo,mabango na utoaji wa vibali vya ujenzi kidigitali na kupunguza usumbufu kwa wananchi kufika Halmashauri kwa ajili ya kupata huduma hizo.
Taarifa hiyo imetolewa leo na Afisa Mipangomiji mwandamizi wa Ofisi ya Rais TAMISEMI, George Miringay katika semina ya mafunzo ya ukusanyaji wa kodi za majengo,mabango na utoaji wa vibali kidigitali kupitia mfumo wa TAUSI, kwa wataalamu wa Halmashauri ya Mji Makambako.
Miringay amesema kuwa, awali huduma ya ukusanyaji wa kodi za majengo na mabango zilikuwa zikitolewa kupitia Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) kwa njia ya analogia na kwa sasa huduma hizo zimerejeshwa OR TAMISEMI na zitakuwa zikikusanywa na watendaji wa mitaa badala ya kuajiri watu wa kukusanya na vibali vya ujenzi vitatolewa na wataalamu kidigitali pasipo mwananchi kufika ofisini.
Amesema kuwa, kupitia mfumo wa TAUSI mwananchi anaweza kupata kibali cha ujenzi ndani ya siku moja tofauti na awali ambapo vibali vilitolewa hata baada ya miezi miwili, kujua kiasi cha gharama anachotakiwa kulipa kwa ajili ya bango pamoja na kodi ya majengo ambayo inakusanywa kupitia luku za umeme kwa sasa.
Pia, amesema kuwa kutokana na baadhi ya majengo kutolipiwa kodi ya majengo kwa kukosa umeme kupitia mfumo wa TAUSI majengo yote yanayotumika wamiliki watatakiwa kulipa kodi baada ya watendaji wa Kata, Mitaa na Vijiji kuwasajili kwenye mfumo isipokuwa nyumba zilizojengwa kwa tope,ofisi na majengo ya Serikali,makanisa, misikiti na nyumba zinazomilikiwa na kanisa au msikiti.
Aidha, amebainisha kuwa kupitia ukusanyaji wa kodi hizo Halmashauri kupitia makusanyo ya kodi za majengo itapata asilimia 20 na asilimia 100 kupitia makusanyo ya ushuru wa mabango ambapo awali fedha hizo zilielekezwa Serikali kuu.
Ametoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa watendaji wanapofika katika maeneo yao kwa ajili ya usajili kwani kodi hizo sio mpya bali ni maboresho yamefanyika kutoka analogia kwenda digitali ili kurahisisha utoaji na upatikanaji wa huduma kwa ufanisi.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa