Na. Lina Sanga
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe leo katika kikao kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji Makambako,baada ya kufanya ziara kwenye baadhi ya maeneo ndani ya Mkoa wa Njombe ikiwa ni pamoja na Halmashauri ya Mji Makambako.
Mhe. Bashe ametoa kauli hiyo baada ya baadhi ya Mawakala wa mbolea waliosambaza mbolea mwaka 2014 na 2015 kuiomba Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kuwalipa madai yao ili waweze kuendeleza biashara zao.
Mhe. Bashe amesema kuwa,kutokana na njia za utoaji wa mbolea za ruzuku kipindi cha nyuma kutokuwa na usimamizi mzuri,kuna baadhi ya watumishi wa Serikali walishiriki katika udanganyifu wa uuzaji wa mbolea hizo kinyume na malengo yaliyokusudiwa kwa kujinufaisha wenyewe na makampuni ya usambazaji wa mbolea pamoja na mawakala badala ya mkulima.
Ameongeza kuwa, kutokana na udanganyifu uliofanyika katika zoezi hilo,Serikali inaendelea kufanya uchunguzi juu ya uhalali wa madai hayo,kwani asilimia hamsini ya madai hayo sio halali na kuna baadhi ya vocha zilighushiwa hivyo malipo yatafanyika baada ya uchunguzi kukamilika.
Aidha,Mhe. Bashe ameifungia Kampuni ya parachichi inayofahamika kwa jina la Kandia Fresh Produces Ltd yenye makao makuu nchini Kenya inayofanya biashara ya ununuzi wa parachichi katika Mkoa wa Njombe , kutojishughulisha na biashara ya parachichi ndani ya nchi ya Tanzania tena ,kwani kitendo walichofanya cha kutupa dampo parachichi walizonunua shambani kwa madai ya kutokomaa ni kitendo cha uonevu kwa wakulima na wameonyesha kukosa uaminifu ambao unaweza kuharibu sifa ya soko la nje la bidhaa hiyo kutoka Tanzania.
Mhe. Bashe amesema kitendo kilichofanywa na Kampuni hiyo ni kitendo kibaya chenye lengo la kukwamisha jitihada za Serikali ya awamu ya sita, za kufungua mipaka ya nchi na kutafuta masoko ya uhakika nchi za nje.
Ametoa wito kwa wakulima wa zao la parachichi kutokuuza matunda ambayo hayajakomaa vizuri na kuzitaka kampuni za ununuzi wa parachichi nchini kutosafirisha matunda yasiyo na ubora ili kutunza soko la zao hilo.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa