Na. Lina Sanga
Serikali kupitia Mradi wa TACTIC ina mpango wa kuipendezesha Halmashauri ya Mji Makambako Kwa ujenzi wa Soko la Kisasa,Stendi ya Mabasi ya kisasa pamoja na bustani ya kisasa kwa ajili ya utalii.
Taarifa hiyo imetolewa leo na Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa alipokuwa akitoa salamu kwa wakazi wa Mji wa Makambako baada ya Mbunge wa jimbo la Makambako,Mhe. Deo Kasenyenda Sanga kutoa ombi kwa Mhe. Samia Suluhu Hassan juu ya ujenzi wa soko la kisasa la Makambako.
Mhe. Bashungwa amesema kuwa,Halmashauri ya Mji Makambako ni moja kati ya Miji 48 ambayo itanufaika na mradi wa TACTIC,ambao lengo kuu ni kupendezesha Miji kwa ujenzi wa miradi mbalimbali ya kisasa.
Ameongeza kuwa,dhamira ya Mhe. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha miundombinu na miradi inayojengwa inaendana na hali nzuri ya wananchi wa nyanda za juu kusini, ili kuwawezesha wananchi kufanya kazi,kufungua mipaka ya nchi pamoja na kuvutia uwekezaji ili kujenga uchumi wa nchi.
Aidha, ametoa shukurani kwa Mhe. Samia kwa kuongeza bajeti ya Wakala wa barabara Vijijini na Mijini (Tarura),kwa asilimia 250 kutoka Mil.800 hadi bil. 2.8 katika bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 na agosti 14, mwaka huu Wakandarasi kwenye kila Wilaya watasaini mikataba kwa ajili ya kazi ya matengenezo ya barabara.
Pia,amemuahidi Mbunge wa jimbo la Makambako, Mhe. Sanga kuwa baada ya kukamilisha ziara ya Rais ombi lake la fedha za ukamilishaji wa zahanati ya Kijiji cha Mkolango litafanyiwa kazi,kwa kumuomba Rais afungue pochi ili zahanati hiyo ikamilishwe.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa