Na. Lina Sanga
Halmashauri ya Mji Makambako inaandaa sheria ndogo kuhusiana na utoaji wa chakula shuleni na usimamizi wa utekelezaji wa mikataba ya lishe ambapo mchakato huo utaanzia ngazi ya wananchi.
Tamko hilo limetolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Makambako Kenneth Haule,katika mkutano wa baraza la madiwani uliofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri,baada ya kuwasilishwa kwa taarifa ya Kamati ya uchumi,afya na elimu inayohusu hali ya utoaji wa chakula cha mchana katika shule za msingi,huku shule zilizopo Mjini zikiwa na idadi kubwa ya wanafunzi wasiopata chakula shuleni tofauti na shule zilizopo Vijijini.
Akiwasilisha taarifa hiyo Mwenyekiti wa Kamati ya uchumi,afya na elimu,Mhe. Imani Fute amesema kuwa maendeleo ya taaluma kwa wanafunzi yanaenda sambamba na maboresho ya miundombinu ya kufundishia pamoja na mpango wa lishe bora kwa watoto,kwa kuhakikisha watoto wote wanapata chakula shuleni.
Mhe. Fute amesema kuwa licha ya faida kubwa za utoaji wa chakula shuleni kwa wanafunzi,takwimu za utoaji chakula cha mchana katika shule za msingi bado haziridhishi,kwani baadhi ya wazazi hasa maeneo ya Mjini hawachangii chakula cha watoto wao shuleni.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Makambako,Kenneth Haule amesema kuwa kutokana na baadhi ya wazazi kukaidi kuchangia chakula cha watoto wao shuleni,Halmashauri inaandaa sheria ndogo kuhusiana na utoaji wa chakula shuleni na usimamizi wa utekelezaji wa mikataba ya lishe kuanzia ngazi ya Kijiji,Mtaa hadi Kata.
“Wazazi wanapaswa kutambua umuhimu wa chakula shuleni,suala sio mtoto apate chakula pekee,suala ni je,anapata chakula kwa muda sahihi? Na ni chakula gani? Jana tumesaini mikataba ya lishe pamoja na Watendaji wa Kata hivyo suala la chakula shuleni tunakoelekea sio hiyari tena itakuwa ni lazima kila mtoto kupata chakula shuleni chenye virutubisho muhimu kwa afya zao ikiwa ni agizo la Serikali”,alisema Haule.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Makambako,Mhe. Hanana Mfikwa ameiagiza Kamati ya uchumi,afya na elimu pamoja na Idara ya elimu Msingi kuchakata uwiano wa miundombinu ya shule na idadi ya wanafunzi,ili kupata uwiano halisi na endapo hakuna uwiano hatua za kuongeza na kuboresha miundombinu zifanyike.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa