Naibu waziri wa Ofisi ya Rais TAMISEMI,Mhe.David Silinde amewaagiza Maafisa elimu idara ya msingi na sekondari,katika halmashauri ya Mji Makambako, kuhakikisha shule shikizi zinapata usajili kuwa shule rasmi pindi ujenzi wa madarasa utapokamilika.
Mhe. Silinde ametoa agizo hilo leo,katika ziara ya ukaguzi wa miradi ya ujenzi wa madarasa inayotekelezwa kwa Fedha ya Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko 19, katika wilaya ya Njombe,ambapo katika halmashauri ya Mji Makambako, amekagua mradi wa ujenzi wa madarasa matatu shule shikizi ya Mlumbe sekondari katika kata ya Lyamkena na ujenzi wa madarasa mawili shule ya msingi shikizi kihanga katika kata ya Mahongole.
Pia amewapongeza wananchi wa kata ya Lyamkena,kwa kutoa fedha kiasi cha shilingi mil. 24,kwa ajili ya fidia ya eneo ambalo limejengwa shule shikizi ya sekondari ya lyamkena inayotambulika kama Mlumbe sekondari,ambayo itasaidia kupunguza mlundikano wa wanafunzi katika shule mama ya Lyamkena sekondari.
Aidha, Mhe. Silinde amemuagiza Mkurugenzi wa halmashauri ya Mji Makambako,Bw. Kenneth Haule kukamilisha madarasa na vyoo vilivyojengwa kwa nguvu ya wananchi katika shule ya msingi shikizi Kihanga,kwa kutumia mapato ya ndani ili shule hiyo ipate usajili kuwa shule ya msingi rasmi.
“Shule hizi shikizi kulingana na idadi ya madarasa yaliyopo,zina sifa ya kupata usajili kuwa shule rasmi ,hivyo maafisa elimu hakikisheni taratibu za usajili zinaanza kwa wakati na TAMISEMI itaongeza idadi ya madarasa mengine,pia halmashauri kupitia mapato yake imalizie majengo haya ya shule ya msingi shikizi kihanga yaliyojengwa kwa nguvu ya wananchi ili kuunga mkono juhudi za wananchi”,alisema Mhe. Silinde.
Mwisho alitoa maelekezo kwa Uongozi wa halmashauri ya Mji Makambako kukamilisha majengo hayo kwa viwango na kuwa miradi yote ya ujenzi wa madarasa inayotekelezwa kwa fedha ya Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Uviko 19, kukamilishwa ifikapo desemba 25,2021 ili kukabidhiwa kwa Mkuu wa wilaya na Mkuu wa Mkoa na hatimaye madarasa hayo kukabidhiwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe.Samia Suluhu Hassan.
Katika Halmashauri ya Mji Makambako, jumla ya shilingi mil.840 fedha ya Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko 19, ilipokelewa kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 26 pamoja na meza na viti kwa shule za sekondari na madarasa 12 pamoja na madawati kwa shule za msingi na bweni moja la wanafunzi wenye mahitaji maalumu shule ya msingi Idofi pamoja na vitanda.
Naye Katibu Tawala Mkoa wa Njombe,Judica Omary ametoa shukurani kwa Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,kwa fedha ya ujenzi wa madarasa kwani kupitia fedha hiyo Upungufu wa madarasa kwa sasa umepungua,na wanafunzi wataingia darasani mwezi januari kwenye madarasa yaliyokamilika na yenye meza na viti pamoja na madawati kwa upande wa shule za msingi.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa