Ili kuhakikisha watoto wa kike wanakuwa salama na kusoma katika mazingira salama, wanajitambua na wanapata elimu sahihi kuhusu afya ya uzazi na haki zao za msingi, Halmashauri ya Mji Makambako leo kupitia divisheni ya maendeleo ya jamii kwa kushirikiana na wananchi,kuelekea maadhimisho ya siku ya wanawake ngazi ya Halmashauri imetoa taulo za kike kwa wanafunzi wa Shule ya sekondari Mtimbwe,iliyopo Kata ya Utengule pamoja na kutoa elimu juu ya kujijali, kujitambua, kujikubali na kujiamini ili kufikia malengo.
Akizungumza na wanafunzi hao Mkuu wa divisheni ya Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Mji Makambako, Bi. Lilian Mwelupungwi amewataka wasichana kutambua thamani yao, na kuhakikisha wanajilinda kiafya na kuhudhuria masomo bila kikwazo chochote.
Afisa Ustawi wa Jamii,Bi. Maria Mkude alipata nafasi ya kutoa elimu juu ya kujijali, kujitambua, kujikubali na kujiamini ,huku akisisitiza umuhimu wa wasichana kuwa na uthubutu wa kujilinda na kutokubali kushawishiwa na watu wanaoweza kuharibu mustakabali wao, kwani Kujitambua ni msingi wa mafanikio.
Naye, Afisa Maendeleo ya Jamii, dawati la msaada wa kisheria,Bi. Amina Ally, ametoa wito kwa wanafunzi kuripoti matukio ya ukatili wa kijinsia na kuikumbusha jamii kuwa, ina wajibu wa kuhakikisha watoto wa kike wanalindwa dhidi ya changamoto zinazoweza kuwakatisha masomo.
Kwa niaba ya walimu wote na uongozi wa shule ya sekondari Mtimbwe, Mwl. Mwangolombe wa Mtimbwe Sekondari ameishukuru Halmashauri ya Mji Makambako pamoja na wanawake wote, kwa kutoa taulo za kike kwa wanafunzi wa shule hiyo, ambazo zitasaidia kupunguza changamoto wanazokutana nazo wasichana kipindi cha hedhi, hivyo kuwawezesha kuhudhuria masomo bila kikwazo.
Maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ngazi ya Halmashauri yatafanyika kesho Machi 6,2025 katika Uwanja wa Polisi na Kilele cha maadhimisho hayo yatafanyika Kijiji cha Bulongwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Makete Machi 8,2025.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa