Na. Lina Sanga
Umoja wa wasafirishaji Mkoa wa Njombe leo, wametoa mashine ya kufulia na vitu mbalimbali kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum katika shule ya msingi Idofi kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha watoto hao wanapata fursa ya kusoma kama watoto wengine.
Akikabidhi mashine hiyo pamoja na vitu vingine kama mikeka, juisi na sabuni, Bw. Burton Salingwa, Mwenyekiti wa Umoja huo amesema umoja huo ulipitia changamoto zinazowakabili watoto hao na wahudumu wanaowahudumia, na wakaamua kununua mashine yenye thamani ya mil. 1.6 yenye uwezo wa kufua na kukausha nguo ili kurahisisha zoezi la usafi.
" Huu ni utaratibu wetu wa kila mwaka na kwa mwaka huu, kupitia mwanachama mwenzetu ndg. Kihwelo tuliona ni vema tuje shuleni hapa ili kuchangia kidogo kupunguza changamoto zilizopo hivyo leo tumetoa vitu vyenye jumla ya Mil. 1.9 na tutarudi tena wakati mwingine",alisema Salingwa.
Mhe. Odillo Fute, diwani wa Kata ya Mlowa kwa niaba ya Kata na uongozi wa shule hiyo, ameushukuru umoja huo kwa kujitoa kwa ajili ya watoto hao na kuwakaribisha tena wakati mwingine wanapopata nafasi kwani watoto hao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali.
Naye, Mwl. Samweli Komba, Afisa elimu divisheni ya awali na msingi katika Halmashauri ya Mji Makambako kwa niaba ya Mkurugenzi ameushukuru Umoja wa wasafirishaji Mkoa wa Njombe kwa kutoa mashine, mikeka na vitu mbalimbali kwa ajili ya watoto na kuwataka wazazi wa watoto hao pamoja na jamii kushirikiana na Serikali kuimarisha ulinzi wa watoto dhidi ya majanga mbalimbali.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa