Na. Lina Sanga
Mkuu wa Mkoa wa Njombe,Mhe. Anthony Mtaka amewaruhusu walimu ndani ya Mkoa wa Njombe, kufungua vituo vya twisheni ili kufundisha wanafunzi baada ya muda wa kazi badala ya kutumia muda huo kwenye vilabu vya pombe na kuendekeza ulevi.
Mhe. Mtaka ametoa ruhusa hiyo leo katika kikao cha uzinduzi wa mwongozo wa vitabu vitatu vya elimu,uliofanyika Shule ya Sekondari Mpechi na kuwataka walimu kuhakikisha wanautumia vizuri muda wa masaa za kazi na watoro watashughulikiwa.
Amesema kuwa daktari anamiliki duka la dawa, zahanati na anahudumia hospitali zaidi ya tatu,mwalimu haruhusiwi kufungua kituo cha kufundishia masaa ya ziada kwa madai hatafundisha vizuri darasani,kitu ambacho sio kweli.
"Mimi sijali wewe una masaa ya wewe na mimi fanya kazi kwa uaminifu baada ya muda wa kazi kuisha utawala binafsi,mwalimu mtoro nitajua jinsi ya kushughulika nae,darasa la saba wanamaliza shule mwezi ujao weka bango ya kufundisha masomo ya sekondari wazazi walipie watoto wasome na wewe ujiongezee kipato,sio kila siku tunaona mabango ya nguvu za kiume mara kusafisha nyota,punguzeni msongo wa mawazo kwani nikikuona baa saa kumi nitakuuliza?,badala ya kukaa kwenye pombe si ufundishe QT?"amesema Mhe. Mtaka.
Ameongeza kuwa walimu wa Mkoa wa Njombe watembee kifua mbele kwani amewaruhusu kufanya kila kitu kwa kufuata sheria,kwani kazi ya ualimu ni haiba na ili kuitunza hawana budi kuanzisha miradi mbalimbali ili kujiongezea kipato na kuachana na mikopo umiza ambayo inawadharirisha wao na taaluma yao.
Ametoa wito kwa wakuu wa shule na walimu wakuu kuwafukuza watu wanaofika shuleni,kwa madai ya kukopesha walimu fedha kwani walimu wengi wanaishi maisha magumu kwa sababu ya mikopo umiza inayokopeshwa mitaani.
Amewataka walimu wote ndani ya Mkoa wa Njombe kutokuwa wepesi wa kukopa mitaani kwenye saccos zinazoanzishwa na watu mitaani na kama wanashindwa wamjulishe ili awatafutie benki nzuri wapate mikopo na kujikwamua kiuchumi.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa