Walimu wa michezo wa shule za msingi na sekondari katika Halmashauri ya Mji Makambako leo, wamepewa semina maalum inayolenga kuwaandaa kwa ajili ya mashindano ya Umoja wa Michezo wa Shule za Sekondari Tanzania (UMISETA) na Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA), ili kuinua viwango vya michezo mashuleni na kuhakikisha washiriki wanakuwa na maandalizi thabiti ya mashindano hayo, ambayo Kitaifa kwa mwaka huu yatafanyika Mkoani Iringa.
Katika semina hiyo iliyofanyika katika viwanja vya michezo vya shule ya sekondari Makambako na kufuatiwa na mafunzo kwa vitendo, walimu walipata mafunzo juu ya mbinu bora za kufundisha na kuendeleza vipaji vya wanafunzi katika michezo mbalimbali kama vile mpira wa mikono, mpira wa wavu, riadha na michezo mingine ya ushindani.
Mwl. Taifa Lumato,Afisa Michezo wa Halmashauri ya Mji Makambako, amewasisitiza walimu hao, kuendelea kuongeza jitihada katika kukuza vipaji vya vijana na kuiweka Makambako katika nafasi nzuri ya kushiriki na kushindana katika mashindano ya hayo.
Naye, Mwl. Katunzi, kutoka shule ya Sekondari ya Mkilima kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo amesema kuwa, mafunzo hayo yamekuwa yenye manufaa makubwa na yatasaidia kuboresha mbinu za ufundishaji wa michezo mashuleni.
Sambamba na mafunzo ya michezo, walimu hao walipata elimu kuhusu msaada wa kisheria kutoka divisheni ya Maendeleo ya Jami juu ya umuhimu wa kuzingatia usawa wa kijinsia kwa walimu pamoja na wanajamii kwa ujumla.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa