Na. Lina Sanga
Wito huo umetolewa leo na Mkuu wa Wilaya ya Njombe,Mhe. Juma Sweda akitoa salamu za Serikali katika Mkutano wa Baraza la Madiwani kwa kipindi cha kuishia Robo ya pili kwa mwaka wa fedha 2025/2026 katika Halmashauri ya Mji Makambako uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Kata ya Lyamkena.
Mhe. Sweda amesema kuwa,ipo haja kwa Kitengo cha mazingira kuandaa program maalum ili kuhamasisha wananchi kupanda miti kwenye makazi yao ili kupunguza athari zinazotokana na upepo mkali kipindi cha mvua kwani kwa sasa Mji wa Makambako unakabiliwa na uharibifu wa mazingira kwa ukataji wa miti kwa kasi na kusababisha ukame unaopelekea ukosefu wa maji.
Pia,amesisitiza utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kutolewa kwa msawazo kwa kila Kata ili kuwafikia walengwa kila Kata pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu mikopo inayotolewa na benki ya NMB na CRDB ambazo ni fedha za Serikali zinazokopeshwa kwa riba ndogo ili wanaokosa fedha zinazotolewa na Halmashauri wakakope benki.
Lakini pia, ametoa rai kwa viongozi wa Mitaa na vijiji kubainisha wanafunzi ambao hawajaripoti shuleni kuhakikisha wanaripoti shuleni kwa kubainisha wanafunzi waliofaulu kujiunga sekondari ni wangapi na wapo wapi, kwa kutambua sharia na sera ya elimu kuwa kila mtoto ana haki ya kupata elimu na kuwataka wazazi kutowatumikisha watoto kwenye kazi kama gereji kwani ni kinyume cha sheria.
Pamoja na hayo ameitaka Halmashauri ya Mji Makambako kuhakikisha miradi viporo yote iliyopokea fedha inakamilika pamoja na kuitaka Halmashauri kuweka mikakati ya kukusanya mapato zaidi kwani Makambako kwa sasa inakuwa kwa kasi na inahitaji mipango mikubwa inayohitaji fedha.
Mwisho ametoa wito kwa sekta ya Afya kuweka mikakati ya namna bora ya kutekeleza sera ya bima ya afya kwa wote ili kuepuka malalamiko ya wananchi,kwani wananchi wanalipa kabla ya kupata huduma na kuagiza sekta hiyo kuandaa mpango kazi wa namna watatoa huduma kwa wananchi.
Naye,Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Makambako Mhe. Robert Shejamabu kwa niaba ya baraza la Madiwani amemuhakikishia Mkuu wa Wilaya kuwa maelekezo yote wameyapokea na wapo tayari kuyafanyia kazi kwa bidii.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa