Na. Lina Sanga
Rai hiyo imetolewa na Mhe. Mario Kihombo,diwani wa Kata ya Mahongole ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya huduma za jamii ya Halmashauri ya Mji Makambako,katika bonanza jumuishi la kitaaluma,michezo na sanaa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum,lililofanyika jana katika shule ya Msingi Idofi.
Mhe. Kihombo amesema kuwa,ushiriki wa wananchi ikiwa ni pamoja na wazazi na walezi wa watoto wenye mahitaji maalum , ni chachu katika kampeni ya kupinga na kutokomeza tabia ya baadhi ya wazazi wanao wafungia watoto wenye ulemavu ndani,kwa kuamini hawana uwezo wa kufanya jambo lolote ikiwa ni pamoja na kuwasomesha.
“Watoto hawa wana uwezo mkubwa wa kujifunza na kuongeza ujuzi katika taaluma, michezo na sanaa,sisi wote tuliopo hapa tumeshuhudia mambo mengi wanayojifunza,tumeona kazi za sanaa walizotengeneza pamoja na ushiriki wao katika michezo mbalimbali,maigizo,uimbaji na masomo ya darasani,haya yote ni kiashiria kikubwa kuwa hali ya ulemavu si kikwazo cha watoto wetu kusoma na kujifunza mambo mbalimbali kwani elimu ni haki ya kila mtu”,alisema Mhe. Kihombo.
Ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan,Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa kutoa fedha zaidi ya Mil. 275 za ujenzi wa mabweni ya kisasa kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum, katika shule ya msingi Idofi na kuwawezesha watoto hao kupata muda zaidi wa kujisomea.
Naye, Bw. Sevelini Mhiliwa,mwenyekiti wa kamati ya shule ya msingi Idofi ameishukuru Serikali kwa kutekeleza ujenzi wa mabweni ya watoto wenye mahitaji maalumu,ambayo yamewezesha watoto kutoka maeneo mbalimbali kusoma katika shule hiyo na kuongeza hadhi ya Mtaa wa Idofi kwa wageni na viongozi mbalimbali kufika katika shule hiyo.
Ametoa wito kwa wazazi na wakazi wa Idofi kutumia fursa ya uwepo wa mabweni hayo kuwafichua watoto wenye mahitaji maalum wanaofichwa ndani ,pamoja na wazazi wanaowataka watoto wao kujifelisha makusudi kwa madai ya kutokuwa na fedha za kuwasomesha , licha ya Serikali kuendelea kuwekeza fedha nyingi za ujenzi wa miundombinu ya elimu ikiwa ni pamoja na madarasa.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa