Na .Tanessa Lyimo
Wanawake wametakiwa kuendelea kuongeza jitihada za kujiletea maendeleo , wakati Serikali ikifanya juhudi za kutengeneza fursa kwa ajili ya wananchi na kuwa na udhubutu wa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, hususani katika Uchaguzi Mkuu unaotarijia kufanyika Oktoba 2025.
Wito huo ulitolewa jana na Mhe. Rosemary Lwiva,diwani wa Kata ya Majengo akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Mhe. Juma Sweda ambaye alikuwa Mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani 2025, ngazi ya Halmashauri ya Mji Makambako, yaliyofanyika katika uwanja wa polisi, katika Kata ya Mwembetogwa.
Mhe. Lwiva amewapongeza wanawake waliojikwamua kiuchumi kwa kupitia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri na kuwataka wengine kujitokeza pindi mikopo hiyo itakapotolewa, pamoja na kuwasisitiza wanawake kutumia fursa za elimu zinazotolewa na jamii kuleta mageuzi katika nyanja mbalimbali za maendeleo.
Aidha, amewataka wanaume kutoa ushirikiano pale wanawake wanapokumbana na mabadiliko mbalimbali siyo tu ya kijamii , bali hata kiafya,kama vile ukomo wa hedhi na kumfanya kutotimiza baadhi ya majukumu katika familia.
Pia ,ametoa wito kwa jamii kuendeleza mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia na kuwataka wanawake kuendelea kujifunza elimu ya haki na usawa katika jamii ,ili kutokomeza dhana potofu zinazoikumba jamii na kujua utaratibu sahihi wa kupata haki zao.
Naye, Mwenyekiti (UWT) Wilaya ya Njombe (CCM), Bi. Beatrice Malekela ameikumbusha jamii kutomsahau na kutomwacha nyuma binti wa kike katika maswala ya uwezeshaji kiuchumi na usawa, kwani uwezeshaji wa mtoto wa kike unaanzia katika ngazi ya familia.
Kilele cha Maadhimisho ya siku ya wanawake duniani 2025 ngazi ya Mkoa wa Njombe yatafanyika Halmashauri ya Wilaya ya Makete,machi 8,2025.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa