Na. Lina Sanga
Mkurugenzi wa huduma za afya, Lishe na Ustawi wa Jamii katoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) , Dkt. Rashid Mfaume amewataka watumishi wa divisheni za Afya nchini,kutokughushi takwimu za watu wanaoishi na maambukizi ya VVU na utekelezaji wa mikataba ya Lishe,kwani kupitia takwimu hizo wanaisababisha Serikali kupanga mipango ambayo si halisia.
Dr. Mfaume alitoa wito huo jana wakati akizungumza na watumishi wa sekta ya Afya katika Halmashauri ya Mji Makambako baada ya kukagua hali ya miundombinu,nyaraka na utendaji kazi kwa ujumla, katika kituo cha Afya Lyamkena,Hospitali ya Mji ya Makambako(Mlowa) na kituo cha Afya cha Makambako.
Dr. Mfaume amesema kuwa,baadhi ya watumishi wanajihusisha na udanganyifu wa takwimu kwa sababu ya kuahidiwa posho ambayo hutolewa baada ya kupatikana kwa watu wenye maambukizi na kuwatahadharisha kuacha vitendo vya upotoshaji wa takwimu hizo kwani sheria kali zitachukuliwa kwa watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo.
Aidha, ametoa rai kwa Maafisa Lishe wote nchini kutofanya udanganyifu wa takwimu kwenye taarifa ya utekelezaji wa mikataba ya lishe kwenye kadi alama, ili kupata rangi ya kijani kwenye mfumo wa lishe,kwani kwa kufanya hivyo wanaipotosha Serikali kupanga mipango ambayo si halisia ya utekelezaji wa afua na viashiria vya lishe .
Ametoa onyo kwa watumishi wote wenye tabia ya kufanya udanganyifu kwenye takwimu kuacha mara moja , na badala yake watoe takwimu sahihi kulingana na uhalisia ili Serikali itoe msaada endapo utekelezaji ni hafifu.
Aidha,ameipongeza Halmashauri ya Mji Makambako kwa utekelezaji mzuri wa ujenzi wa miundombinu ya Afya na Kumpongeza Dkt. David Ng'umbi anayetoa huduma katika jengo la dharura (EMD) kwa ubobezi wa utoaji wa huduma za dharura.
Pia,amewataka wakaguzi wa ndani wote nchini kutoa mrejesho wa ukaguzi walioufanya kwa taasisi husika na kutokufanya ukaguzi pekee yao.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa