Na. Lina Sanga
Watumishi wa Umma na Sekta binafsi wametakiwa kuanzisha miradi ya maendeleo kabla ya kustaafu , ili kupata uzoefu na kutambua changamoto za mradi mapema badala ya kutumia kiinua mgongo kuanzisha miradi.
Rai hiyo imetolewa leo na Mhe. Anthony Mtaka , Mkuu wa Mkoa wa Njombe katika sherehe za maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani 2024 katika Viwanja vya sabasaba Mkoani Njombe.
Mhe. Mtaka amesema watumishi wanatakiwa kutumia fursa zilizopo katika maeneo wanayoishi kwa kufanya uwekezaji, ikiwa ni pamoja na kumiliki ardhi,kujenga nyumba na kuanzisha miradi mahali walipo hata kama sio kwao kabla ya kustaafu.
“Watumishi chochote unachotamani kukifanya baada ya utumishi wako,niwaombe sana tuanze kuvifanya saizi tukiwa ofisini, ukistaafu utatamani parachichi za wiki mbili zikomae uuze” alisema Mhe. Mtaka.
Aidha, ametoa rai kwa watumishi kununua magari kwa ajili ya matumizi yao binafsi,badala ya kugombania magari ya Serikali na kujengeana chuki zisizo na ulazima na kuwataka watumishi kujiepusha na roho mbaya ya kuoneana wivu usio na tija katika maisha ya utumishi na binafsi.
Pia, amewataka viongozi wanaofanya maamuzi kuhusu watumishi wa umma kuwa mfano mzuri kwa maisha yao binafsi,na kuwataka watumishi kuchukua mikopo kwenye benki na kuachana na mikopo ya kausha damu.
Mwisho amezipongeza taasisi za kidini na elimu katika mkoa wa Njombe kwa kuisukuma ajenda ya lishe ili kutokomeza udumavu, na kutoa wito kwa jamii na familia kuwaelekeza vijana masuala ya familia na uzazi ili kutokuwa na vijana wasiotambua majukumu ndani ya familia.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa