Na. Lina Sanga
Uelewa mdogo wa wazazi na walezi kuhusu umuhimu wa elimu kupitia Mpango wa Elimu ya Msingi Kwa Waliokosa (MEMKWA),ni kikwazo kikubwa cha watoto waliokosa elimu kwa mfumo rasmi kujiunga na MEMKWA.
Hayo yameelezwa na mwalimu wa MEMKWA shule ya Msingi Juhudi,Mwl Rose Mhema katika maadhimisho ya wiki la elimu ya watu wazima,yaliyofanyika leo katika viwanja vya shule ya msingi Kahawa katika Halmashauri ya Mji Makambako.
Mwl.Mhema amebainisha kuwa kutokana na mwamko hasi wa wazazi na walezi juu ya kuwasomesha watoto walikosa elimu kwa mfumo rasmi kujiunga na MEMKWA, imepelekea watoto kufanya maamuzi ya kujiandikisha bila ridhaa ya wazazi na kukosa vifaa vya kujifunzia.
“Mtoto mwenye miaka kumi ambaye amekosa elimu kwa mfumo rasmi,wazazi hawaoni umuhimu wa kuwaandikisha elimu ya MEMKWA hali inayosababisha watoto kujileta shuleni wenyewe,wanapofika shuleni walimu wanawapokea lakini wanakabiliwa na changamoto ya kukosa vifaa vya kujifunzia,kutokana na wazazi kutoona umuhimu wa kuwasomesha watoto wao,hivyo walimu wanalazimika kuwanunulia vifaa ili kuwasaidia kuanza masomo yao”,alisema Mwl. Mhema.
Aidha amesema kuwa,licha ya mwamko hasi wa wazazi na walezi kumekuwa na mafanikio makubwa kupitia MEMKWA, kwani idadi ya watoto wasio jua kusoma na kuandika imepungua,na wanafunzi wengi wamefanikiwa kujiunga na masomo ya sekondari hadi vyuo.
Ametoa wito kwa Serikali kupitia ofisi ya Mkurugenzi kuwapunguzia majukumu walimu wa MEMKWA,kwani wana kazi nyingi tofauti na walimu wa elimu rasmi.
Mpango wa Elimu ya Msingi Kwa Waliokosa (MEMKWA) ulianzishwa rasmi mwaka 2003,kwa lengo la kuwawezesha watoto wote kuanzia miaka tisa hadi kumi na nane ambao hawakupata nafasi ya kujiunga darasa la kwanza katika mfumo rasmi kutokana na changamoto mbalimbali kupata elimu.
Halmashauri ya Mji makambako ina jumla ya vituo kumi vya MEMKWA, ambavyo ni shule ya msingi Lyamkena,Makambako,Kifumbe,Juhudi,Ikwete, Mtanga,Majengo,Kilimahewa,Magegele na Mludza.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa