Na. Lina Sanga
Waziri wa Nchi,ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama ameipongeza halmashauri ya mji makambako kwa kufikia asilimia 95 ya kufanya malipo kwa kutumia mifumo ya malipo ya fedha ya Serikali kwa wanufaika wa TASAF pamoja na Ujenzi wa miradi wenye viwango.
Mhe. Jenista ametoa pongezi hizo leo katika kijiji cha Ikelu, kata ya Utengule alipofanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya ujenzi wa zahanati ya kijiji cha ikelu na ujenzi wa nyumba pacha za watumishi wa kituo hicho iliyojengwa kwa fedha za Tasaf.
Amesema kuwa malipo ya fedha kupitia mifumo ya Serikali ni maelekezo ya mheshimiwa Rais,ili kuhakikisha usalama wa matumizi ya fedha za Serikali na wanufaika wote kupata fedha kwa wakati.
Ameiagiza TASAF makao makuu kuhakikisha wanaongeza juhudi na kuimarisha mifumo yake pamoja na kusimamia zoezi la malipo ya fedha kwenda kwa walengwa kitaifa linafanyika,ili kiwango cha utekelezaji kiongezeke kutoka asilimia ishirini zilizopo sasa na walengwa wapate fedha zao kwa wakati na usalama.
Pia,ametoa wito kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Makambako kuhakikisha mikopo ya asilimia kumi inayotolewa kwa vijana,wanawake na watu wenye ulemavu zinawafikia walengwa wa TASAF kupitia vikundi vyao vya maendeleo vya TASAF, pamoja na kuwatambua watoto wanaotoka kaya masikini wanaohitimu elimu ya msingi na Sekondari na kushindwa kuendelea na masomo ya vyuo ili kuwapatia nafasi ya kujiunga vyuo vya kati (VETA) kwa kusomeshwa bure na Serikali.
Aidha,amewapongeza wananchi wa Kata ya Utengule kwa uzalendo wa kuchangia zaidi ya Mil 16. 7 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje na nyumba ya watumishi,na kuwata wananchi wote nchini kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kuchangia shughuli za maendeleo katika maeneo yao.
Ametoa wito kwa kaya masikini ambazo zinanufaika na TASAF kutumia fedha wanazopata vizuri na kuzalisha,kwani matarajio ya Serikali ni kuziwezesha kaya hizo kuweza kusimama vizuri na kuweza kujitegemea ili Serikali ipate nafasi ya kuzisaidia kaya nyingine.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa